WAZIRI AWESSO AAGIZA MGAWO WA MAJI MWANZA

 


Waziri wa Maji, Jumaa Awesso (kushoto)akipata maelezo kutoka kaimu Meneja Ufundi wa MWAUWASA, Salim Losimbilo (wa pili kutoka kulia) alipotembelea na kukagua mitambo ya kusukuma maji Mabatini ambayo imepata hitlafu na kusababisha upungufu wa maji kutoka uzalishaji wa lita milioni 90 hadi 90 kwa siku.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Awesso, leo alipotembelea kituo cha mitambo ya kusumuma maji Mabatini baada ya kupata hitlafu.
**********************
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Bodi ya Maji ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mwanza (MWAUWASA) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo,Mhandisi Leonard Msenyele imeagizwa kupanga ratiba maalumu ya mgawo wa maji  na kuwawezesha wananchi waishio maeneo ya miinuko kupata huduma ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Awesso ametoa maagizo hayo leo baada ya kutembelea mitambo ya kusukuma maji Mabatini  iliyopata hitlafu ya mota mbili kuungua na hivyo kuathiri na kushusha kiwango cha uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 90 hadi 80 kwa siku na kuonya hatakubali kusikia mgawo wa upendeleo.

Amesema hitlafu iliyotokea katika mitambo hiyo ya kusukuma maji  imewathiri zaidi wananchi wanaoishi katika maeneo ya miinuko  kwa kukosa huduma ya maji, na hivyo kuiagiza  bodi na uongozi wa MWAUWASA kuweka mgawo wa haki sawa katika maeneo hayo wapate huduma. 

“Nimeridhika kwa namna wataalamu na watendaji wanavyojitahidi kufanya ukarabati kurejesha kiwango cha uzalishaji maji kwa sababu hitlafu iliyotokea  imesababisha upungufu wa lita milioni 10 za maji, wananchi wanaoishikatika miinuko  hawana huduma ya maji.Naagiza Bodi na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA kuweka ratiba maalumu ya mgawo  wa maji,”amesema Awesso.

Waziri huyo wa maji amesema Rais Samia Suluhu Hassan hataki kusikia taharuki ya maji kwa wananchi hivyo wizara na MWAUWASA itahakikisha changamoto hiyo inakwisha na kuwaomba wananchi wa Jiji la Mwanza wawe watulivu ambapo wizara itahakikisha mitambo inaimarishwa kwa kuikarabati ili kurejesha kiwango cha maji.

“Sitakubali mgawo wa maji wa upendeleo,nahitaji kuona wananchi wa kwenye miinuko wanapata huduma ya maji kwa ubora na kwa wakati,kwa sababu ya hitalafu iliyotokea katika mitambo, hatuwezi kukubali wananchi wakose maji hasa katika miiunko, wekeni ratiba maalum maana maji hayana mbadala ,wananchi wakikosa maji hayo maisha yao yanakuwa hatarini,”amesema.
Awesso amesema watalaamu wa MWAUWASA hawalali wanahangaika usiku na mchana kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha ili wananchi wanaoishi katika miinuko wanapate huduma ya maji kwa usawa kulingana na ratiba ya mgawo itakavyopangwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post