Na. Catherine Mbena/MKOMAZI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeishauri serikali kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa miradi inayotekelezwa na taasisi za uhifadhi ili fedha hiyo iweze kutumika kufanya kazi kubwa zaidi ya kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii.
Akizungumza katika majumuisho ya ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mwenyekiti wa Kamati Daniel Sillo (MB) alisema,
“Serikali iangalie uwezekano kwa siku zijazo kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili kutopunguza fedha za utekelezaji. Tungepata msamaha wa kodi tungefanya kazi kubwa sana na kwa muda mfupi hivyo ni vizuri kuangalia hili kwa taasisi za uhifadhi.”
Wakitoa maoni katika majumuisho hayo baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo walipongeza kazi nzuri na kubwa iliyofanywa na TANAPA katika kusimamia miradi ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO -19.
“Tumeona jinsi ambavyo vitu vinafanyika katika ubora na tunaona nia njema ya kufikia malengo ya nchi. Katika taarifa ya matumizi na ulipaji wa fedha kwa wakandarasi unaona kazi kubwa sana iliyofanyika lakini malipo hajafanyika, hii inamaanisha kwamba TANAPA wameweza kutafuta wakandarasi wenye uwezo.” alisema Mhe. Issa Mtemvu.
Aidha, walisema maboresho ya miundombinu hii yanaenda sanjari na juhudi za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ya kutangaza utalii wa nchi yetu na fursa za uwekezaji nchini.
Akitoa shukrani kwa Kamati, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini - TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Waitara alisema “Tumefurahi mmeona umuhimu wa miradi hii katika hifadhi zetu na tunashukuru sana kwamba mtatusemea ili tupate zaidi na tuweze kuboresha zaidi.”
Waitara alibainisha kwamba magari na mitambo iliyonunuliwa itatawanywa katika kanda nne za hifadhi ili kusaidia maboresho ya miundombinu ya hifadhi.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana aliwashukuru wajumbe kwa kutenga muda wa kuja kutembelea miradi na kuwaomba kuendelea kuunga mkono juhudi za wizara ili kufikia adhma ya serikali ya watalii milioni tano na mapato ya dola za kimarekani bilioni sita.
Aidha, Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, William Mwakilema alisema kuwa kwa namna ambavyo Mhe. Rais ameonyesha njia kwa kutangaza utalii kupitia filamu maarufu ya “The Royal Tour Tanzania” ni wajibu wetu kuhakikisha mazingira wanayotembelea watalii yameboreshwa.
Kamishna Mwakilema aliwahakikishia wajumbe wa kamati kuwa amepokea maelekezo yao kwa niaba ya Menejimenti na kuahidi kufanya kazi usiku na mchana kutekeleza majukumu ya kusimamia rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilitembelea hifadhi ya Taifa Tarangire,Mkomazi na Kilimanjaro kuona utekelezaji wa Miradi ya maendeleo na mapambano dhidi ya UVIKO-19.