Mh,Anthony Mavunde asisitiza ujenzi maabara ya mbolea kuharakishwa







                          .................................

 Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania kuhakikisha kuwa ujenzi wa maabara ya Mbolea unakamilika kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo, alipotembelea ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ili kuona hatua ya ujenzi wa maabara hiyo ulipofikia.

Naibu Waziri Mavunde amesema kukamilika kwa jengo hilo la maabara kutaifanya Tanzania kuwa na maabara kubwa inayojihusisha na upimaji wa mbolea  Afrika mashariki na kati.

Aidha, ameitaka kamati ya ujenzi pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi wa TFRA kuhakikisha wanasimamia ipasavyo upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ili ifikapo mwezi Agosti ujenzi wa maabara hiyo uwe umekamilika.

“Suala la ujenzi mwisho iwe mwezi wa saba, mwezi wa nane nitafika ili kuona hatua mliyofikia kwani serikali ina shauku kubwa kuona maabara inafanya kazi hivyo mfanye kazi usiku na mchana”, Mavunde alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Dkt. Stephan Ngailo alisema ofisi yake itahakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati kwani kukamilika kwake kuna manufaa kwa nchi, taasisi anayoisimamia na jamii ya watanzania kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa ma baraaba hiyo Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja, Joseph Charos amesema ujenzi umekamilika kwa asilimia 70 na kuwa tayari vifaa vyote kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo vimenunuliwa.

Ujenzi wa maabara hii ni katika kuhakikisha TFRA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa mbolea na kuzisajili kwa matumizi ya kilimo,  kufanya uchambuzi wa udongo na mimea pamoja na kuitambulisha maabara kimataifa kutokana na uwezo wake katika kuchambua mbolea Afrika Mashariki naKati.

Post a Comment

Previous Post Next Post