Imeelezwa kuwa utaratibu uliowekwa ili kisimamia utoaji wa mbolea ya ruzuku kwa wa kulima kwa msimu ujao wa kilimo hautatoa mianya ya ubadhirifu kwa mtu yeyote ili kujinufaisha na mbolea hizo isivyo.
Katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mifumo ya ruzuku iliyopita serikali imeandaa mfumo wa kielektroniki wa usajili wa waingizaji, wasambazaji, wauzaji wa mbolea pamoja na wakulima wanaotarajiwa kunufaika na mbolea hizo za ruzuku.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha kumepambazuka cha Redio One kilichokuwa hewani kuanzia saa 2:15 hadi saa 3:15 asubuhi leo tarehe 19 Julai, 2022.
Amesema mfumo huo utatumika katika kuhakikisha huduma zote za usambazaji wa mbolea za ruzuku unatolewa na mtu sahihi na kumfikia mkulima mwenyewe na si vinginevyo.
Akizungumzia namna usajili utakavyofanyika, Dkt. Ngailo amesema Usajili utafanywa na Afisa ugani waliopo katika ngazi za kata na vijiji na kudhibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji na baadaye taarifa za mkulima kuingizwa kwenye mfumo wa kielectroniki ili kuwezesha usambazaji wa mbolea hizo.
Ameongeza kuwa mzalishaji au mwingizaji wa mbolea nchini atatumia mifuko maalum kwa ajili ya ruzuku yenye QR code na maandishi yanayosomeka ruzuku ili kuutambulisha kuwa mbolea hiyo inanunuliwa na mkulima kwa bei ya ruzuku.
Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye kipindi hicho, Kaimu Meneja wa Uingizaji wa Mbolea Kwa Pamoja kutoka TFRA, Elizabeth Bole amesema utoaji wa ruzuku za mbolea si jambo jipya nchini isipokuwa serikali imeendelea kuboresha mifumo ya utoaji wa mbolea hizo ili kuondoa mianya ya ubadhilifu ili wakulima halisi waweze kunufaika vilivyo na ruzuku hiyo.
Aidha, Bole amebainisha kuwa mnufaika wa mbolea ya ruzuku ni yule tu aliyesajiliwa kwenye mfumo wa kielektroniki wa ruzuku ambapo mkulima atasajiliwa kwa jina, kijiji anachoishi, ukubwa wa eneo la shamba na hivyo kutoa picha halisi ya kiasi cha mbolea kunachohitajika kwa ajili ya shamba lake.
Utoaji wa ruzuku za mbolea ni matokeo ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuona umuhimu wa kuwawezesha wakulima kulima kwa tija na kupelekea uhakika wa mavuno ya chakula na biashara kwa ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.
Kiasi cha shilingi bilioni 150 za kitanzania zimetengwa ili kutumika kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.