Serengeti Girls imeibeba Afrika- Mhe. Mchengerwa

Na John Mapepele.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema kwa mara ya kwanza historia imeandikwa kwa timu ya soka ya wanawake ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Girls) kuitoa kimasomaso Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla baada ya kufuzu kuingia akwenye mashindano ya dunia baada ya kuibamiza Cameroon jana kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika Zanzibar.

Akizungumza wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2022/23 ya Wizara yake bungeni leo, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa timu zote za Taifa katika michezo mbali mbali, kuiga mfano wa Serengeti Girls kwa kupambana kufa na kupona, kwa ari na uzalendo kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa lao.

Ameongeza kuwa Serengeti Girls  imetimiza  ndoto  ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na watanzania ya kuiingiza Tanzania kwenye  historia  ya kushiriki  kwenye  mashindano ya kombe la dunia ambapo haijawahi kutokea  katika  nchi yetu kabla na baada ya uhuru wake.

“Hakika haikuwa kazi rahisi hata kidogo, hasa ukizingatia kwamba nchi ya Cameroon ni nchi iliyobobea na yenye historia kubwa katika mchezo wa mpira wa miguu jambo ambalo lingeweza kuwaogofya wachezaji wetu.

Serikali chini ya Uongozi na maelekezo thabiti ya Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha timu hiyo inapata ushindi na kufuzu, tuliwajengea matumaini, tulitengeneza na kuzalisha chembe chembe za uzalendo na Utaifa mioyoni mwao ili kuwapa ari ya kushinda katika michuano yao ya kimataifa hususani katika michezo yao miwili ya mwisho dhidi ya Cameroon.” Amesisitiza, Mhe Mchengerwa       

Pia amesema ushindi huo umeipa heshima nchi yetu na kuiwezesha kufuzu kushiriki katika michuano ya kombe la Dunia kwa Wanawake wenye umri chini ya miaka 17 itayofanyika nchini India.

“Hongereni Sana Serengeti Girls, Hongera Sana Mhe. Rais, Hongereni sana Wanawake wote wa Tanzania, Hakika Mmetuheshimisha” amehitimisha Mhe. Waziri


 

Post a Comment

Previous Post Next Post