BODI YA WADHAMINI TANAPA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MIRADI YA UVIKO- TARANGIRE

Na. Catherine Mbena/TARANGIRE

Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ilikagua na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Tarangire ambapo ukarabati wa barabara, viwanja vya ndege pamoja na ununuzi wa mitambo umefanyika kupitia Mradi wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa miradi hiyo tarehe 29.06.2022 Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA,
Jenerali (Mstaafu). George Waitara aliipongeza Menejimenti ya Hifadhi za Taifa kwa kazi nzuri ya usimamizi wa miradi hiyo

“Naona tupo vizuri na tuendelee kufanya kazi kwa kujituma zaidi ili kama kuna fungu jingine nina hakika ni rahisi kupewa.
Simamieni kwa umakini mkubwa hii miradi ili iwe na ubora uliokusudiwa kulingana na thamani ya pesa ilivyotumika alisema Waitara

Naye, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Kamishna Nsato Marijani alipongeza kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati huku ikizingatia thamani ya pesa

“Kukamilika kwa wakati kwa miradi hii ni kazi kubwa sana imefanyika, kiwango cha kazi kinalingana na thamani ya pesa, hii ni dhahiri kwamba kuna usimamizi mzuri wa miradi”

Awali, akiwakaribisha wajumbe wa bodi katika Hifadhi ya Taifa Tarangire Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, William Mwakilema alibainisha umuhimu wa miundombinu hiyo katika ustawi wa utalii nchini ambapo kwa muda mfupi Hifadhi imeshuhudia ongezeko kubwa la wageni.

Bodi ya wadhamini wa TANAPA inaendelea na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya uboreshaji miundombinu katika Hifadhi za Taifa Mkomazi na Kilimanjaro.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post