Serikali Kuendelea Kuboresha Huduma Za Kijamii Kwa Wananchi Waliopisha Maeneo Ya Hifadhi

 Mwandishi wa NCAA, Arusha.


Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Hifadhi pamoja na wale waliohama kwa hiari ili kupunguza shughuli za Kibinadamu ili kuimarisha Uhifadhi na utalii katika maeneo hayo.

Maelezo hayo yametolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Tanzania Dkt. Maurus Msuha wakati akitoa mada kwenye kikao na Waandishi wa Habari kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Juni, 2022.

Kikao na wanahabari hao kilikuwa na lengo la kutoa uelewa kuhusu zoezi la uwekaji wa alama katika pori tengefu la Loliondo na zoezi la Wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga.

Amebainisha kuwa katika eneo la pori tengefu la Loliondo lililokuwa limehifadhiwa na Serikali lina ukubwa wa kilomita za mraba 4000 lakini baada shughuli na mahitaji ya wananchi wa vijiji vilivyoko karibu na pori hilo kuongezeka Serikali iliamua kumega na kuwaachia wananchi eneo lenye Kilomita za mraba 2500 na kuamua kuweka alama za mipaka eneo lililobaki lenye Kilomita za Mraba 1500 kwa ajili ya shughuli za Uhifadhi.

“Serikali kutenga eneo la kilomita za mraba 2500 na kuwapa wananchi wake inatoa fursa kwa wananchi kujengewa huduma za kijamii kama Malambo, majosho, huduma za maji, barabara, vituo vya afya, shule pamoja na kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi ” amefafanua Dkt. Msuha.

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka amebainisha kuwa taarifa zilizoripotiwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kuna Ng’ombe wamekufa baada ya kuhamia Kijiji cha Msomera hazina ukweli na kueleza kuwa picha hizo ni za Ng’ombe waliokufa katika nchi ya Jirani kutokana na matatizo ya ukame mwaka 2018.

Ameongeza kuwa kuwa zoezi la wananchi wa Ngorongoro wanaohamia kwa hiari kwenda Msomera linaendelea vizuri na wananchi wameendelea kuhamaiska na kujitokeza kujiandikisha, aidha kundi la tatu la wanachi wa Ngorongoro lenye kaya zaidi ya 25 linatarajiwa kuhamia msomera siku ya alhamis ya wiki hii.

Ngorongoro na Loliondo ni sehemu mbili tofauti zilizohifadhiwa na Serikali ambapo Loliondo ni eneo linalowekwa alama za mipaka ili kutofautisha shughuli za uhifadhi na maeneo ya wananchi.
Aidha zoezi linalofanyika katika Hifadhi ya Ngorongoro ni jambo la hiari

linalohusisha wananchi kuhama kwa hiari yao wenyewe kwenda Kijiji cha Msomera Mkoani Tanga ambapo Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wananchi hao.


Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Tanzania Dkt. Maurus Msuha akifafanua jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu zoezi la uwekaji wa alama katika pori tengefu la Loliondo na zoezi la Wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga,kwenye kikao na Waandishi wa Habari kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Juni, 2022.



Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka akizungumza kwenye kikao Maalimu na Waandishi wa Habari kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Juni, 2022,akieleza kuhusu taarifa zilizoripotiwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kuna Ng’ombe wamekufa baada ya kuhamia Kijiji cha Msomera ambazo hazina ukweli na kueleza kuwa picha hizo ni za Ng’ombe waliokufa katika nchi ya Jirani kutokana na matatizo ya ukame mwaka 2018.

Post a Comment

Previous Post Next Post