Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi ameelekeza mradi wa ukarabati wa tuta la kuzuia majichumvi katika Bonde la Ukere Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kusini, Pemba ukamilike haraka ili kuwapa fursa wananchi kuendelea na kilimo cha mpunga.
Ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara akiambatana na Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Thabit Idarous Faina pamoja na watendaji wao katika eneo hilo kwa ajili ya kukagua Mradi wa Urejeshaji Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS).
Mitawi aliyemwakilisha Katibu Mkuu Bi. Mary Maganga alisema kuwa kitendo cha ucheleweshaji wa mradi huo kinasababisha wananchi katika maeneo mengine yakose fursa ya kutekelezewa mradi kama huo.
Alionesha kushangazwa na kuchelewa kuanza kwa ukarabati wakati tayari Serikali ilishatoa fedha kupitia mradi huo muda mrefu ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika eneo hilo zilizosababisha majichumvi kutoka baharini kuingia kwenye bonde hilo.
“Tutakumbuka eneo hili kabla lilikuwa likitumika kwa kilimo cha mpunga lakini baadaye liliharibiwa na mvua Ofisi ya Makamu wa Rais ikaombwa kusaidia kutatua changamoto hii kwa kukarabati tuta hili,” alisema Mitawi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Thabit Idarous Faina alitaka uandaliwe mpango kazi utakaoonesha shughuli hizo zitakamilika baada ya muda gani.
Faina alisema kuwa mpango kazi huo utasaidia kuona nini kinakwamisha mradi ili kuweza kupatia ufumbuzi na hatimaye wananchi waendelee na shughuli za kilimo cha mpunga kama awali.
Alimtaka Mratibu wa Mradi wa LDFS katika Wilaya ya Micheweni Bw. Abdallah Hamad Faki pamoja na watendaji wengine kufunga mikanda ili ili uweze kukamilika haraka kwa kuwa bonde hilo linatoa ajira kwa wananchi.
Hata hivyo mratibu huyo alidai kilichokwamisha ilikuwa ni ukosefu wa njia ya kufikisha malighafi katika eneo walilopaswa kujenga tuta.
Mratibu wa Mradi Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Joseph Kihaule alisema shughuli ya ukarabati wa tuta ulipaswa kuanza tangu Machi 2022 kwasababu tayari fedha zilishapelekwa.
Alisema kuwa kimsingi shughuli hiyo ilipaswa kutekelezwa kwa kutumia force account kama ilivyokubalika, ili iende kwa haraka lakini bado inaonekana kucheleweshwa.
Sehemu ya tuta la kuzuia majichumvi kutoka baharini kuingia katika Bonde la mpunga la Ukere Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kusini, Pemba ambalo ni miongoni mwa matuta yanayokarabatiwa kupitia Mradi wa Urejeshaji Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS
Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Katibu Mkuu Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Thabit Idarous Faina pamoja na watendaji wao wakiwa katika ziara ya kukagua ukarabati wa tuta la kuzuia majichumvi kwenye Bonde la mpunga la Ukere Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kusini, Pemba unaotekelezwa kupitia Mradi wa Urejeshaji Ardhi iliyoharibika na kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS)