WATUMISHI 52 WA TANAPA WAHITIMU MAFUNZO YA JESHI LA UHIFADHI

 

Na. Edmund Salaho/MKOMAZI.
Watumishi 52 wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wamehitimu mafunzo ya mabadiliko ya utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao kufanya kazi katika mfumo wa jeshi la uhifadhi. 
 
Awali, akisoma taarifa ya mafunzo hayo, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara-TANAPA, Herman Batiho alisema mafunzo hayo yalihusisha askari wa Uhifadhi 50 na maafisa Uhifadhi wawili 
 
lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi na kuimarisha usimamizi wa rasilimali zilizopo katika maeneo ya hifadhi.
Akifunga mafunzo hayo, Kamishna wa Uhifadhi-TANAPA, William Mwakilema amewataka watumishi hao kutekeleza kwa vitendo mbinu na maarifa waliyoyapata kwenye mafunzo hayo kwa maslahi ya taifa. 
 
“Ni tegemeo langu kwamba mafunzo haya yamewajengea uzalendo, uadilifu, ujasiri , utayari, kujiamini, na ari kubwa katika kulinda rasilimali za taifa. Niwapongeze sana mmeonyesha kwa vitendo na mkatekeleze kwa vitendo yote mliyojifunza.” alisema Mwakilema.

Kamishna Mwakilema amewatahadharisha “Silaha ni chombo ambacho kinatakiwa kitumike kwenye shughuli za ulinzi na matumizi yake yawe sahihi. Silaha zitumike pale tu unapokabiliwa na tukio ambalo linaweza kuhatarisha au kupoteza maisha yako.” 
 
Aidha, Kamishna Mwakilema alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na wakufunzi wa mafunzo hayo katika kuwajengea uwezo wahitimu hao kusimamia na kulinda Rasilimali za Wanyamapori
na Misitu.





Post a Comment

Previous Post Next Post