Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Hassan Abbasi leo Mei 3, 2022 wameungana na Viongozi Wakuu wa Nchi na waumini wa dini ya Kiislamu kushiriki Swala ya Eid El Fitri iliyofanyika kitaifa katika Msikiti Mkuu wa BAKWATA Kinondoni Muslim Jijini Dar es Salaam.
Swala hiyo imeongozwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu. Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa.
Katika Swala hiyo, Mufti wa Tanzania ametoa wito kwa waislam wote nchini kujitokeza na kushiriki kikamifu zoezi la kitaifa la Sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu nchini.
Mufti Zubeir amefafanua kwamba muislam kukataa kuhesabiwa kwa kigezo kuwa kitendo cha kuhesabiwa ni haramu siyo msingi wa dini ya kiislam na kuwataka kushiriki kikamilifu zoezi hilo kwa maendeleo ya taifa letu kwa ujumla.
Sensa ni zoezi muhimu kwa taifa lolote duniani kwa kuwa linasaidia Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo kwa ufanisi.