Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni Sanaa ana michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kutawakatia BIMA ya afya washindi wote wa Tuzo za muziki 2021 kwa muda wa mwaka mzima ili kuwaondolea adha ya kupata matibabu wakiwa katika shughuli zao za muziki na nje ya nchi.
Mhe. Mchengerwa amesema haya wakati wa usiku wa kilele cha utoji wa Tuzo za Muziki 2021 kwenye Ukumbi wa kimataifa wa Julis Nyerere jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo.
Aidha, amesema Serikali pia itawakatia pensheni wasanii wote washindi walioshinda tuzo hizo na kuwalipia kwa mwaka mzima ikiwa ni mwanzo wa kuwaanzishia mfumo wa kujiwekea akiba uzeeni ili kuwaondolea adha ya kuwa ombaomba pindi kipindi chao cha kazi kinapofikia ukingoni.
“Na hapa niseme tu ni lengo la Serikali yetu ya Awamu ya Sita (6) chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wasanii, wanamichezo na wadau wa Sanaa wanawekewa mazingira mazuri ya ufanyaji kazi na mazingira mazuri ya hapo baadae baada ya kustaafu kazi. Hivyo, licha ya zawadi hii ya BIMA na Pensheni kwa washindi wa leo hapa, lakini tayari Katibu Mkuu, ameanza mazungumzo na taasisi zetu za bima na pensheni ili mwishowe wasanii, wanamichezo na wadau wetu wote wa tasnia za sanaa na michezo waweze kunufaika na bima na pensheni kwa njia rahisi ili kuyalinda maisha yao ya sasa na ya badae” Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Amelitaka Baraza la Sanaa la TAaifa (BASATA) kutenda haki na kujiepushe na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na kwamba lisitumike kukandamiza haki za Wasani na kuwagawa wasanii na kusababisha makundi miongoni mwao.
“Wito wangu BASATA ni chombo cha kuwaunganisha wasanii na kutetea Haki na maslahi ya wasanii na kuwa kimbilio la Wasanii." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema hatakubali kuona vitendo viovu vikiendelea wakati wa uongozi wake.
Kwa upande wa Taasisi ya Hakimiliki (COSOTA) Mhe, Mchengerwa ameiagiza kuwasaidia wasanii kusajili kazi zao ili waweze kunufaika nazo.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe, Samia Suluhu Hassan amepewa Tuzo ya Heshima kwenye usiku huo wa kilele cha utoaji wa tuzo za muziki Aprili 2, 2022 jijini Dar es Salaam.
Tuzo hiyo ya heshima amepewa na wasanii kwa kuthamini mchango wake mkubwa anaoutoa kwa wasanii nchini.
Tuzo hiyo imepokewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa kwa niaba yake.
Watu wengine waliopata tuzo za heshima katika usiku wa utoaji wa tuzo ni pamoja na Diamond Platnumz, Ruge Mutahaba, Bibi Kidude na Mkuu wa majeshi.
Katika usiku huu tuzo 51 zimetolewa ambapo nne (4) ni za heshima na arobaini na saba (47) ni za kupigiwa kura.
Wakipokea tuzo hizo, washindi wamepongeza juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasaidia wasanii na kurejesha tuzo hizo za muziki ambazo zilipotea kwa takribani miaka sita.