UJENZI WA BARABARA YA IGAWA HADI TUNDUMA WAIVA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi,Mhandis Godfrey Kasekenya, akijibu swali katika mkutano wa saba wa Bunge unaoendelea, jijini Dodoma.

………………………………………..

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilometa 218 ikiwa ni maandalizi ya kuifanyia ukarabati kwa kiwango cha lami.  

Akijibu swali Bungeni leo la Mhe. Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge Viti Maalum, Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza kuwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umekamilika hivyo taratibu za manunuzi zinaendelea ili kuanza ujenzi huo.

Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza kuwa ukarabati na upanuzi wa barabara ya Igawa hadi Tunduma utafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili kuwa njia nne kwa sehemu ya Uyole – Ifisi yenye urefu wa kilometa 29.  

Ameongeza kuwa taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa barabara hiyo zinaendelea na inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha, Kasekenya amesema katika ujenzi huo pia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umejumuisha barabara ya mchepuo katika Jiji la Mbeya sehemu ya Uyole – Songwe Bypass yenye urefu wa kilometa 48.9 ili kupunguza msongamano katikati ya jiji la Mbeya.

Amemhakikishia Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mbeya Mhe. Fyandomo, kuwa wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara sehemu ya Uyole – Ifisi watalipwa fidia zao kabla ya ujenzi kuanza.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki inayokwenda katika Bwawa la Julius Nyerere, Naibu Waziri Kasekenya amemhakikishia Mbunge wa jimbo la Morogoro Kusini, Mhe. Hamis Taletale, kuwa maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo yanaendelea.

Post a Comment

Previous Post Next Post