BALOZI PINDI CHANA “AKOSHWA’’ UTENDAJI KAZI TANAPA



 
 Na. Edmund Salaho/TANAPA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameeleza kufurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA), ikiwemo ukusanyaji wa mapato pamoja na juhudi za kujitangaza licha ya changamoto ya ugonjwa wa UVIKO- 19 ulioikumba dunia mwishoni mwa mwaka 2019.

Waziri Chana, ametoa pongezi hizo alipotembelea makao makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), jijini Arusha kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo katika ziara yake yenye lengo la kutambua maeneo ya kazi.

Awali, akimkaribisha Mhe. Waziri, Kamishna wa Uhifadhi-TANAPA, William Mwakilema alimweleza mafanikio mbalimbali ya Shirika hilo ikiwemo juhudi zinazofanywa na TANAPA katika kuimarisha ulinzi na usalama wa rasilimali pamoja na wanyamapori, uboreshaji wa huduma za utalii, utekelezaji wa mfumo wa Jeshi la Uhifadhi pamoja na ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza na Menejimenti hiyo Mhe. Balozi Dkt. Chana licha ya kuwapongeza watumishi wa TANAPA kwa utendaji wao amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo ambao sasa ni Jeshi la Uhifadhi kuonesha utofauti katika utendaji wao kutoka wa kiraia kuwa wa kijeshi.

“Nawapongeza TANAPA na kuwaasa mkiwa ni Jeshi la Uhifadhi muoneshe tofauti ili jamii ione kuwa kweli kulikuwa na sababu ya kuomba Jeshi la Uhifadhi, na wananchi waone kuwa ni Jeshi ambalo limekuwa likiwasaidia na kuwaokoa” alisema Balozi Dkt.Chana

Aidha, Balozi Dkt. Chana alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaonesha mfano mzuri katika utekelezaji wa masuala mbalimbali hususani utalii.

“Mhe Rais wetu amekuwa kinara katika kutangaza utalii kupitia kampeni ya “Royal Tour”alisema Balozi Chana

Pia, Balozi Chana ameahidi kuendeleza ushirikiano na kufanyakazi kwa pamoja ili kuweza kutekeleza mipango waliyojiwekea kwa faida ya watanzania ambapo ameahidi ushirikiano uliotukuka na kusisitiza kuwa katika kipindi chake cha uongozi hakutakuwa na urasimu.

Balozi Pindi Chana yupo ziarani kutambua maeneo ya kazi katika taasisi zote zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Post a Comment

Previous Post Next Post