Mhe Mchengerwa , Trans Innova na M- Nichan Group wakubaliana kuwekeza Kwenye Sanaa na Michezo


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo Aprili 7, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka Kampuni ya Trans Innova na  M-Nichani Group zote kutoka nchini India na kukubaliana kuwekeza katika sekta za Sanaa na Michezo.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam ambapo wawekezaji hao wameonesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta za utamaduni, sanaa na michezo.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Mchengerwa amewashukuru  wawekezaji hao kwa kuwa tayari kuunga mkono sekta hizo ambazo ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi kwani zinatoa ajira kwa vijana wengi.

"Tunaahidi kushirikiana na nyinyi ili kukuza sekta hizi na kupitia Chuo cha Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSuBa) tutaweza kufanikisha hili kwani tuna mpango wa kukijenga ili kiwe kituo cha mafunzo ya sanaa na filamu Tanzania", alisema Mhe. Mchengerwa.


Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa M-Nichani Group Bwana Manohar Nichani amesema Tanzania ni nchi nzuri yenye nafasi kubwa ya kukua kiuchumi kupitia sekta ya filamu nchini.

Amesema  India ikiwa ni moja ya nchi inayoongoza katika uzalishaji wa filamu watakuwa tayari kuleta wataalamu kwa ajili ya kutoa mafunzo na kufundisha namna ya kufanya filamu kwa kutumia teknolojia za kisasa na kwa bajeti ndogo.

Ameongeza kuwa wako tayari kuunga mkono ujenzi wa nyumba changamani ambapo itakuwa mji maalum kwa ajili ya kutengeneza filamu hapa nchini,  na pia ujenzi wa studio kubwa na za kisasa maalum kwa ajili ya utengenezaji wa filamu.

"Tanzania ina maeneo mazuri ya wasanii kuweza kufanya maigizo yao na hicho ndicho kilichotuvutia, tutaleta wataalam wetu na waigizaji wakubwa kutoka India kuja kujionea uzuri wa Tanzania na maeneo wanayoweza kuigizia filamu zao" amesema Manohar Nichani.

Naye Dkt. David Faria, ambaye ni Mkuu wa Mipango na Ubunifu kutoka katika kampuni ya  Trans Innova amemweleza Mhe. Waziri nia yao ya kutaka kuinua Sekta ya Michezo nchini ambapo wamekubali kuja kujenga kituo maalum chenye viwanja vya michezo kwa ajili ya mafunzo ambapo hii itahusisha kuchukua vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini na kuwapa mafunzo katika eneo hilo.

Wawekezaji hao wanatarajia kukutana na waigizaji, wazalishaji na waandishi wa filamu nchini siku ya jumamosi tarehe 9 Aprili, 2022 ili kuweza kubadilishana ujuzi


 

Post a Comment

Previous Post Next Post