****************
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko leo tarehe 09 Aprili, 2022 amewavisha vyeo Makamishna wasaidizi waandamizi watano (5) na Makamishna wasaidizi kumi na wawili (12) wa TAWA waliopandishwa vyeo kufuatia maamuzi ya Bodi yaliyofanyika katika kikao chake cha 20 kilichofanyika hivi karibuni mkoani Arusha.
Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku na kuwavisha vyeo Makamishna hao iliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro Mej. Jen. Semfuko amewataka Makamishna hao kuwa mfano katika mazingira yote na kuboresha utendaji kazi wao ili uendane na vyeo vyao.
Aidha Mwenyekiti huyo amewaagiza Makamishna hao kutatua changamoto zinazozunguka maeneo yao ya kazi na migogoro ya wananchi ili kuongeza ufanisi katika shughuli za uhifadhi.
“Makamanda na wapiganaji huko mnakokwenda tunategemea kuona mabadiliko makubwa, hatutegemei kuona migogoro na wananchi, hatutegemei kuona kwamba maeneo yetu yanavamiwa, hatutegemei kuona wananchi wananyanyaswa bila sababu” amesema
Kuhusu upandishwaji wa vyeo, Semfuko amesisitiza kuwa Bodi ya Wakurugenzi TAWA kwa kushirikiana na vyombo vingine inaandaa utaratibu utakaokuwa wa uwazi, ufanisi, usio na usiri na wenye uadilifu mkubwa.
“Hatutaki kuwe na usiri katika upandishwaji vyeo, tunataka katika upandishwaji vyeo ujue kabisa kwamba mimi kwa vigezo, masomo niliyonayo na chochote nitakachokiweka ili kufanya uende ngazi ya pili kiwe kinajulikana” amesema.
“Tunataka kabisa katika utaratibu wetu ujue kama mimi nimepanda leo, baada ya miaka minne au mitatu nikifanya moja, mbili, tatu baada ya miaka mitatu uwezekano wa kuwa cheo hiki ni mkubwa” ameongeza.
Meja Jenerali Semfuko pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro ambaye hivi karibuni alihamishwa na Rais Samia Suluhu kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, kwa uongozi wake mahiri uliosababisha TAWA kupata mafanikio makubwa.
“Pia nitumie fursa hii kumpongeza Waziri wetu wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana kwa kuaminiwa na kuteuliwa na Rais kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunaahidi kumpa ushirikiano pamoja na taasisi zote anazosimamia ili kazi zote za uhifadhi zifanyike kwa maslahi ya taifa na vizazi vya sasa na vijavyo,” aliongeza.
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, akizungumza katika maelezo yake ya awali, alisema uteuzi wa viongozi hao waliovalishwa vyeo vipya umefanyika kwa mujibu wa Muundo wa Shirika na Amri za jumla za jeshi la Uhifadhi, amri namba 5 kwa kuzingatia fani, uwezo wa kuongoza, uadilifu na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
Alitumia nafasi hiyo kuipongeza Bodi ya TAWA kwa kwa uteuzi wa viongozi hao, kwamba una umuhimu kwa sababu unalenga kufanya ugatuzi wa majukumu yaliyokuwa yanatekelezwa na Makao Makuu kwenda kwenye ngazi ya Kanda.