Maafisa Michezo simamieni vikundi vya mazoezi- Mchengerwa


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amewaagiza maafisa michezo nchi nzima kuvisajili vikundi vyote vya mbio za hisani (Marathon) katika wilaya zao na kuvifuatilia ili kutoa motisha kwa vikundi vinavyofanya vizuri na  kuwaandaa wanariadha  kushiriki mashindano ya kimataifa na kusaidia kuzuia maradhi mbalimbali.

Mhe, Mchengerwa ametoa agizo hilo leo, Aprili 10, 2022 wakati akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mbio za hisani kwa ajili ya utoaji wa elimu na ufahamu kuhusu usonji zilizo andaliwa na taasisi ya Usonji ya Lukiza.

Ameongeza kuwa wanariadha hao bora watakaopatikana kupitia mbio mbalimbali watashiriki mashindano ya kimataifa na kuliletea taifa medali mbalimbali.

Akizungumzia mashindano ya Jumuiya ya madola, Waziri Mchengerwa amesema washiriki wote watakao kwenda kushiriki katika michezo hiyo Serikali inawahudumia, na wote wapo kambini wakiendelea kujiandaa vyema kuwakabili washindani wao katika mashindano hayo.


Sisi kama Serikali tumeamua kwamba wachezaji wetu watakaa kambini kwa takribani miezi kwa gharama ili wapate maaandalizi bora ya kiwango cha kimataifa. Mategemeo yetu ni kwamba warudi na medali za ushindi na ninasisitiza katika kipindi changu hakuna wacheza kwenda kutalii bali kushiriki mashindano na kushinda” amefafanua Mhe, Mchengerwa.

Ametoa wito kwa Watanzania wenye uwezo wa kufundisha michezo mbalimbali kujitokeza kutokana na uhaba wa makocha wa michezo hapa nchini.

“Hatuna makocha kabisa tukianzia kwenye Mpira wa Miguu na michezo mingine kwahiyo tuna kazi kubwa kama Wizara kwenda kuwandaa watanzania ili tuweze kupata makocha wa kutosha.” Amesema Mhe, Mchengerwa.

Mbio hizo zilikuwa zimegawanyika katika makundi matatu ya Kilometa 21, Kilometa 10 na kilometa 5 na kuwashirikisha zaidi ya wanariadha 800.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post