Mwandishi Wetu,
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka ameliomba Shirika la Nyumba la Taifa – NHC kuwekeza zaidi jijini humo kwa kujenga nyumba na majengo makubwa ya biashara ambayo yatabadilisha mwonekano wa sasa wa Jiji hilo.
Mtaka amesema kuwa imani kubwa aliyonayoya ya utendaji kazi wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC Nehemiah Mchechu ni wazi kuwa Jiji la Dodoma linakwenda kubadilika kwani majengo makubwa ambayo yatajengwa katika kipindi hiki yatasaidia kulifanya jiji la Dodoma kuwa la kisasa zaidi.
Mtaka ameyasema hayo leo (tarehe 29/03/2022) kufuatia mwaliko wake wa kukutana na Mkurugenzi Mkuu Mchechu ili kubadilisha naye uzoefu kwa ajili ya uendelezaji wa jiji la Dodoma.
Amesema kitendo cha Serikali kuhamishia Makao Makuu yake Dodoma ni dhahiri kuwa jiji la Dodoma linahitajki kubadilika kwa kuwa na majengo makubwa ya kisasa ambayo yatasaidia kukuza uchumi wa nchi na kuonesha uhalisia wa jiji.
“Mchechu nina imani kubwa sana na wewe katika masuala ya ubunifu na uendelezaji miji, nikuombe sasa ufikirie kulibadilisha jiji hili kwa kutujengea majengo makubwa ya kisasa ambayo yatalipa hadhi jiji letu kwa kuwa sasa limekuwa na wageni wengi wakubwa wa Kimataifa ambao wanafika hapa,” amesema Mtaka.
Ameongeza kusema kuwa Kamati ya ujenzi ya jiji pamoja na wote wanaohusika na masuala ya uendelezaji wa jiji letu wako tayari kwa ajili ya kushirikiana na NHC katika kuhakikisha Dodoma ya leo inakuwa mpya zaidi. Tuitumie ardhi yetu vizuri kwa kujenga majengo makubwa ya biashara na nyumba za makazi ambazo zitaendana na hadhi ya Makao Makuu ya nchi.
“Mchechu miji ya wenzetu imeendelea sana na hata ile ambayo imehamisha Makao Makuu ya nchi zao pembezoni mwa miji ikiwemo Abuja na imebaidilisha kabisa mandhari ya miji hiyo na kuifanya kuwa ya kisasa zaidi, ni imani kuwa hata sisi Tanzania tunaweza, NHC tumieni fursa hiyo” amesema Mtaka.
Kwa upande wake Mchechu amemshukuru Mkuu wa Mkoa huyo kwa imani aliyonayo kwake na Shirika kwa ujumla na kuahidi kuwa ataitumia fursa aliyompatia katika kuliendeleza jiji la Dodoma.
Bw. Mchechu ameahidi kuwa wiki ijayo atarudi tena Dodoma hivyo atatumia fursa hiyo kukutana na uongozi wa jiji ili kuweza kuona ni kwa namna gani wanaweza kushirikina na NHC katika kuendeleza jiji la Diodoma.
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Anthony Mtaka akizungumza na Mkurugenzi Mkuu Nehemiah Mchechu ofisini kwake leo.