MKUU WA MKOA DODOMA AHIMIZA WAFANYABIASHARA KUTOA USHIRIKIANO KWA TRA

 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka amewataka Wafanyabiashara mkoani hapo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanaoanza Kampeni ya utoaji elimu kwa Mlipakodi ya Mlango Kwa Mlango yenye lengo la kuwapa elimu ya kodi na kusikiliza kero za wafanyabiashara na kuzitatua.

Akiongea leo ofisini kwake, Mhe. Mtaka amesema kuwa, wafanyabiashara waondokane na hofu ya kuwaogopa maafisa wa TRA wanaowatembelea katika maduka yao na kuwapa elimu ya kodi.

Ameongeza kuwa, fursa ya TRA kuwatembelea wafanyabiashara hao katika maduka yao waitumie ipasavyo ili zoezi hilo liweze kuwa na tija kwa wafanyabiashara mkoani hapo kama ilivyo katika mikoa mingine.

 

“Wafanyabiashara walichukulie hili jambo katika mtazam chanya, watoke kwenye hofu kwamba ukimuona mtu wa TRA unakimbia, hviyo rai yangu kwao waitumie hii fursa vizuri waulize maswali na kutoa kero zao”, alisema Mtaka.

 

Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Bw. Philipo Eliamini amesema kwamba baadhi ya wafanyabiashara wamekua na changamoto zinazowakabili katika biashara zao kwahiyo lengo kubwa la zoezi hilo ni kuwatembelea na kusikiliza changamoto hizo na kuzitatua ikiwemo kujenga mahusiano mazuri katika ya TRA na wafanyabiashara ili kodi iweze kukusanywa kwa hiari.

 

“Rai yetu tunawaomba wafanyabiashara wa Dodoma muwe huru kuuliza maswali, kutoa maoni na kutaja kero zenu ili tuweze kuzitatua ili muwe walipakodi wazuri lakini mkumbuke kutoa risiti za EFD kila mnapofanya mauzo yenu”, alisema Eliamini.

 

Naye Mbunge ambaye pia ni Balozi wa Kodi wa Hiari, Mhe. Zulfa Omary Mmaka pia ametoa rai yake kwa wafanyabiashara mkoani hapo kuitikia wito wa kutoa ushirikiano katika zoezi la elimu kwa mlipakodi lililoanza mkoani hapo.

 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea na kampeni yake ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango ikiwa na lengo la kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kukuza wigo wa walipakodi nchini ambapo zoezi hilo kwa sasa lipo katika mikoa ya Dodoma na Manyara kuanzia leo tarehe 07 Machi, 2022 hadi tarehe 19 Machi, 2022.

 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka (mwenye shati jeupe) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao walimtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuanza zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango mkoani hapo.

Mbunge na Balozi wa Kodi wa hiari, Mhe. Zulfa Omary Mmaka (kushoto) akiteta jambo na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bi. Kabula Mwemezi wakati zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango lililoanza leo mkoani Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akitoa neno kwa timu ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao wako mkoani hapo kwa ajili ya zoezi la utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango lililoanza leo mkoani hapo.


Post a Comment

Previous Post Next Post