Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amemtaka Mkandarasi wa Jengo la Wizara la Mtumba jijini Dodoma kuongeza kasi ya ujenzi na kufanya kazi mchana na usiku ili kwenda na ratiba hatimaye kukamilisha ujenzi wa Jengo hilo kwa wakati uliopangwa kwa kuwa Serikali omeshatoa fedha kwa ajili ya kazi hiyo.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo Machi 21, 2022 wakati alipotembelea kukagua eneo la ujenzi wa Ofisi hizo ambapo hakuridhishwa na kasi ya ujenzi unavyoendelea kwa kuwa upo nyuma ya muda.
Ujenzi huo wa ghorofa 6 unatekelezwa na Mkandarasi Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) chini ya Mkandarasi Mshauri Wakala wa Majengo nchini (TBA).
"Naomba sana Mkandarasi uchape kazi, hakuna sababu ya wewe kutokwenda na ratiba ya kazi zako kwa kuwa Serikali imeshatoa fedha zote za kazi hiyo" Amehoji Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande mwingine, amesema amesikitishwa kuona taasisi za Serikali zimeaminiwa na kupewa dhamana na Serikali kutekeleza mradi huo lakini hazifanyi kazi vizuri.
Amewataka viongozi wa Mkandarasi na Mshauri Elekezi kufika mara moja kwenye eneo la ujenzi ili kukagua maendeleo ya ujenzi huo na kuchukua hatua za haraka za kurekebisha disari zote kabla ya wizara kuwaandikia barua.
Aidha, amemtaka Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wake uendane na wizara nyingine ili uzinduzi rasmi utakapofanywa na viongozi wakuu ufanyike kwa pamoja.