MADARAKA NYERERE ASHUKURU WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

 


Mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere akizungumza kuhusu Maadhimisho ya Miaka 100 ya Mwl Nyerere yanayotarajiwa kufanyika Aprili 13,2022 Butiama mkoani Mara.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,  Juma Mkomi akizungumza na wajumbe wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere mkoa wa Dodoma mzee Antony Mavunde akichangia hoja kwenye kikao cha kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Hayati baba wa Taifa.

Wajumbe wa kamati ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Hayati baba wa Taifa Mwl Nyerere wakiwa kwenye kikao cha maandalizi.

……………………………

Na Sixmund Begashe.


Wizara ya Maliasili na Utalii nchini imepongezwa kwa maamuzi ya  kuandaa maadhimisho makubwa ya miaka miamoja tangu kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere jambo ambalo litazidi kuamsha Ari na hamasa kwa jamii ya kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa.

Hayo yamesemwa na mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Madaraka Nyerere katika kikao maalum cha maandalizi ya maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika  Aprili 13, 2022 wilayani Butiama Mkoani Mara.

Madaraka Nyerere aliongeza kuwa, kwao ni faraja kubwa kuona namna Wizara hiyo imeweka mpango wa miaka 10 ya kuhakikisha inamuenzi Mwl. Nyerere kwani katika kipindi hicho jamii itajengewa uelewa mpana kuhusu maisha ya Baba wa Taifa na kizazi kilichopo kuendeleza utamaduni huo.

Akiendesha kikao cha kujadili utekelezaji wa majukumu ya kamati ndogo ya maandalizi ya adhimisho la Miaka 100 ya Mwl Nyerere (Mwl@100) Jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasi na Utalii, Juma Mkomi licha ya kuzipongeza kamati hizo kwa kazi nzuri pia amezitaka ziongeze kasi ya kufanikisha maadhimisho hayo.

”Japokuwa mnaendelea  kufanya vizuri kwenye maandalizi ni watake muongeze kasi ya maandalizi kwa ubora mkubwa maana Hayati Baba wa Taifa ni Tunu ya Taifa letu pia kimataifa, hivyo ni lazima tumuenzi kwa kishindo kikuu na ninawataka wanakamati wote kushiriki matukio ya maadhimisho yanayoendelea sasa”. Amesisitiza.

Mratibu Mkuu wa Maadhimisho hayo Dkt. Kristowaja Ntandu akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kamati zote, amesema kuwa  maandalizi yanaendelea vizuri akitaja baadhi ya shughuli zinazoendelea kufanyika kuelekea maadhimisho hayo ambazo Makongamano, mijadala ya mada mbalimbali na matamasha.

Naye Mkazi wa Mkoa wa Dodoma Mzee Antony Mavunde ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere mkoani humo licha ya kuupongeza uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua adhimu ya kumuenzi Mwl. Nyerere, ametaja hatua hiyo ni zaidi ya sadaka maana maadhimisho hayo yatapanda mbegu kwa jamii hasa vijana juu ya uwelewa kuhusu urithi wa Hayati Baba wa Taifa.

Adhimisho hilo ni sehemu ya Mpango wa miaka 10 wa Kuenzi na Kusherehekea Urithi wa Utamaduni unaotokana na Maisha ya Mwalimu Julius Nyarere ambao kwa nyakati mbalimbali litakuwa likiadhimishwa kila mwaka Aprili 13  na Wizara ya Maliasili na Utalii

Post a Comment

Previous Post Next Post