WAZIRI DKT. NDUMBARO AAHIDI KUKUTANA NA WADAU WA UWINDAJI WA KITALII WANAOMILIKI VITALU VYA UWINDAJI MWEZI FEBRUARI

 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa pamoja na ujumbe alioambatana nao kutoka Tanzania wakiwa  katika moja ya banda la Tanzania wakiwa na   mmiliki wa Kampuni ya uwindaji wa Kitalii anayemiliki vitalu vya uwindaji nchini Tanzania, Adam Clements (wa pili kulia)  akiwaonesha kwenye kompyuta mpakato moja ya vitalu  hivyo anavyovimiliki mara baada ya Waziri kumtembelea kwa lengo la kujifunza na kusikia changamoto anazokabiliana nazo  katika katika banda lake  ikiwa ni miongoni mwa Makampuni nane kutoka Tanzania yaliyoshiriki katika mkutano wa  50 wa mwaka  wa Uwindaji wa Kitalii ( Annual Hunting Convention) ulioanza rasmi leo  katika Jiji la  Las Vegas, Nevada nchini Marekani.  Wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa TAWA, Brigedia Jenerali,( Mst.)  Hamisi Semfuko  apamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (wa tatu kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Brigedia Jeneralia (Mst.) Hamisi Semfuko ( watatu kulia)  wakipata maelezo kutoka kwa moja ya Wenyeji wa Mkutano wa  50 wa mwaka  wa Uwindaji wa Kitalii ( Annual Hunting Convention), Judith Henkel (wa kwanza kulia) akiwa na mwenzake Anna Saint (wa pili kulia) jinsi wanavyopata Washiriki wa Maonesho ya Uwindaji wa Kitalii  yanayoendelea  kufanyika   katika Jiji la  Las Vegas, Nevada nchini Marekani. Wengine ni Wajumbe aliombatana nao kutoka kutoka Tanzania.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa pamoja na ujumbe aliombatana nao kutoka Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja na  mmoja ya  Wadau wa Uwindaji wa Kitalii John James pamoj na mkewe Julieth Nathians ikiwa ni miongoni mwa Makampuni nane kutoka Tanzania yaliyoshiriki katika mkutano wa  50 wa mwaka  wa Uwindaji wa Kitalii ( Annual Hunting Convention) unaoendelea kufanyika  katika Jiji la  Las Vegas, Nevada nchini Marekani.  Wa nne kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, wa tatu kushoto  ni Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Brigedia Jeneral,(Mst) Hamisi Semfuko.

………………………………………………..

Na Mwandishi Maalum, Las Vegas, Marekani  

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa ahadi ya kukutana na Wadau wa Uwindaji wa Kitalii wanaomiliki Vitalu vya Uwindaji nchini Tanzania ambao sio wanachama wa Chama cha Uwindaji wa Kitalii Tanzania  (TAHOA), Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini hapa Las Vegas Nevada, Marekani wakati  akitoa wito kwa Kamati ya watu 10 aliyoiounda kwa ajili ya kumshauri yeye kama  Waziri  namna bora ya kuendesha sekta ya uwindaji ya kitalii kuwasilisha ripoti itakayomsaidia kuboresha minada ya kielektroniki ya Biashara ya uwindaji wa Kitalii inayofuata hapo baadae.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, mkutano huo utakuwa na lengo la kuboresha mazingira ya biashara ya sekta hiyo ikiwemo uzoefu walioupata katika ushiriki wa Maonesho ya 50 ya mwaka ya Uwindaji wa Kitalii yanayoendelea yakiwakutanisha watunga sera na wafanya maamuzi kutoka nchi mbalimbali Duniani juu ya kuendeleza sekta ya uwindaji.

Akizungumzia juu ya Kamati aliyoiunda Juni 23, 2021 Jijini Dodoma  ya watu 10  ikiwa na watu  watano kutoka Sekta binafsi na wengine  watano kutoka Serikalini kushindwa  kuwasilisha ripoti ya  ushauri huo hadi leo.

Dkt. Ndumbaro amewataka Wadau hao wanaomiliki vitalu vya uwindaji vya kitalii nchini Tanzania kuacha kulalamika baadala yake wawasilishe ripoti hiyo ya ushauri kwa kuonesha yale waliyokubaliana kwa pamoja na yale waliyotofautiana ili yeye kuifanyia kazi ripoti hiyo

Amesema kitendo cha Kamati hiyo kushindwa kuiwasilisha ripoti hiyo kwa wakati kumempelekea  yeye kama Waziri katika wakati mgumu katika kufanya maamuzi yenye maslahi mapana pande zote mbili yaani kwa Serikali na Wadau wa Sekta hiyo.

Amesema kuwasilishwa kwa ripoti hiyo mapema  kutatoa muelekeo wa namna bora ya kuendesha minada ya kielektoniki ya Uwindaji wa Kitalii inayofuata katika mazingira bora zaidi.

“Baadhi yenu mmekuwa mkilalamika tu kuwa hamtaki minada wa kielektoniki wa vitalu vya uwindaji wa Kitalii, leteni ushauri kupitia ripoti hiyo  mkionesha sababu na njia mbadala kama Serikali nini tufanye” alisema Dkt. Ndumbaro.

Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro amewasisitiza Wadau hao waliopo nchini Marekani ambao ni Washiriki wa Maonesho hayo 50, kuiwasilisha ripoti hiyo mapema iwezekanavyo ili mwanzoni mwezi Februari aweze kuitisha mkutano wa Wadau hao.

Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro amewapongeza Wadau hao kwa maoni mazuri waliyoyatoa katika kikao alichofanya nao  nchini hapa huku akiwasisitizia kuuweka ushauri huo katika maandishi na kuwasilisha ofisini kwake  kwa lengo  kuiwezesha Serikali na wadau hao kunufaika kupitia Biashara hiyo.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Uwindaji wa Kitalii (TAHOA), Michel Matheakis alimshukuru Waziri kwa kuwa muumini wa mazungumzo na kuahidi kuwa ripoti hiyo itawasilisha kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

Post a Comment

Previous Post Next Post