AZAM MEDIA YAINGIA MAKUBALIANO NA TTB KUTANGAZA UTALII




                  *******************************

Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) leo Januari 18, 2022 imeingia mkataba wa ushirikiano na Azam Media Limited wa kuandaa kipindi maalumu kitakacholenga kuutangaza utalii wa taifa hili ndani na nje ya Tanzania.

Tukio hilo la kuweka saini kwenye mkataba huo wa ushirikiano, limefanyika katika ofisi za Azam Media zilizopo Tabata Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wa TTB, Jaji mstaafu Thomas Mihayo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando.

“Utalii ni jambo mtambuka ambalo linagusa maisha ya kila mmoja, sasa sisi kama bodi peke yetu hatuwezi. Hauwezi ukazungumzia utalii bila kutangazwa” alisema Jaji mstaafu Mihayo.

“Utalii lazima utangazwe, unatangaza kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na TV na ndio hasa lengo kubwa la TTB kuingia katika mazungumzo na Azam TV” aliongeza Jaji mstaafu Mihayo.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando, amesema ushirikiano huo na TTB utaanzisha kipindi kipya kitakachoitwa “SHANGAZA” kikiwa na lengo la kuushangaza ulimwengu.

“Tunataka kuushangaza ulimwengu, yale mazuri ambayo Tanzania yanayo, yale mazuri ambayo tunaweza kuyaonesha kwa ulimwengu na wenzetu” alisema Tido.

Mkataba huo uliongiwa leo ni wa kipindi cha mwaka mmoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post