MKANDARASI APEWA MIEZI MIWILI KUKAMILISHA MRADI WA CHALINZE NAMBA 3

 Afisa mtendaji mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amemtaka mkandarasi anaetekeleza mradi wa Chalinze namba tatu kukamilisha mradi huo unatarajiwa kuhudumia vijiji zaidi ya 67 wilayani humo kuhakikisha wanakamilisha na kuukabidhi serikalini mradi huo kufikia tarehe 31 mwezi Machi huku akisisitiza kuwa DAWASA imejipanga kutafsiri maono na maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za uhakika za maji.


Akizungumza na Waandishi wa habari katika maeneo tofauti Mhandisi Cyprian Luhemeja amesisitiza mambo mawili, ikiwemo moja la kukamilika kwa mradi wa Mlandizi-Chalinze-Mboga ambapo kwa sasa utakabidhiwa wakati wowote kutoka sasa huku mradi wa Chalinze namba 3 ukiwa katika hatua nzuri na kuwataka wakandarasi wanaoutekeleza kuhakikisha wanaumaliza mradi huo kabla ya tarehe 31 mwezi wa tatu


"Hapa tupo Chamakweza, katika mradi wa Mlandizi-Chalinze-Mboga, na kama mnavyoshuhudia mradi huu umekamilika tunasubiri kukabidhiwa tu....Mradi huu umegharimu Shilingi za kitanzania bilioni 18". Alisema Luhemeja

" Tunawapongeza sana watanzania, kwani hizi bilioni 18 kwa kweli zimetokana na makusanyo yetu wenyewe ya ndani, wanalipa ankara vizuri na kwa wakati na kutuwezesha kukamilisha mradi huu. Hongereni sana watanzania". Aliongeza Luhemeja

Aidha akizungumzia mradi wa Chalinze namba tatu Luhemeja alisema

" mradi huu umechukua muda mrefu sana. Wakandarasi wa awali waliuvuruga na sasa tunao wakandari wapya ambao kwa kweli wanaenda vizuri. Nimewaomba hapa wafanye iwavyo itakavyokuwa kufika tarehe 31 mwezi machi wawe wamekabidhi mradi huu". Alisema Luhemeja

Luhemeja alisema kuwa mradi huo unaogharimu bilioni 100 unagharamiwa kwa ushirikiano baina ya Tanzania na benki ya Exim kutoka India

"Mradi huu ni mkubwa sana na utakuwa tiba ya changamoto ya maji kwa maeneo mengi yaliyokadiriwa na upembuzi wa mradi, utahudumia zaidi ya vijiji 67'',alisema Luhemeja.
Afisa Mtendaji Mkuu Dawasa Cyprian Luhemeja akizungumza na Waandishi wa habari eneo la Chalinze Mboga
Mhandisi Cyprian Luhemeja akikagua tenki la chamakweza Chalinze mkoani Pwani
Afisa Mtendaji Mkuu Dawasa Cyprian Luhemeja akizungumza na Timu ya wataalamu aliongozana kwenye Ziara ya kukagua miradi

Post a Comment

Previous Post Next Post