MPANGO KABAMBE UPELEKAJI NISHATI VIJIJINI WABAINISHWA



 Na Veronica Simba

Imeelezwa kuwa Mpango Kabambe wa Kupeleka Nishati Vijijini umelenga kuwanufaisha wananchi kupitia usambazaji umeme pamoja na nishati bora ya kupikia.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya viongozi wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Kigoma.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy, walisema kuwa Mpango huo unahusisha nishati za aina mbalimbali, siyo umeme peke yake.

Wakili Kalolo alisema kuwa, ni jukumu la REA kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata nishati safi na zenye gharama nafuu ili ziwasaidie kuboresha maisha yao, hivyo Wakala umejiwekea mikakati ya kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa ipasavyo.

Akifafanua, alisema kuwa REA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na inaendelea kufanya vema katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hivyo hakuna shaka katika utekelezaji wa miradi ya aina nyingine za nishati zilizofanyiwa tafiti, utakuwa wenye ufanisi pia.

Akitoa mfano, alisema kuwa tafiti zinaonesha eneo jingine muhimu

linalopaswa kupewa kipaumbele ni katika nishati ya kupikia ambapo asilimia kubwa ya waathirika ni wanawake, ambao kutokana na matumizi ya kuni, wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa ya macho na kifua.

Alisema, ni kwa sababu hiyo, Wakala umedhamiria kuondoa adha hiyo katika jamii hususani wanawake waishio vijijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu akidadavua zaidi kuhusu Mpango huo kabambe, alieleza kuwa umejikita katika sehemu mbili kubwa ambazo ni usambazaji umeme pamoja na nishati ya kupikia.

Alieleza zaidi kuwa, hivi sasa, Wakala unaongeza nguvu zaidi katika nishati ya kupikia ili kuhakikisha kwamba wananchi hususan wa vijijini,

wanatumia nishati bora kwa shughuli za kupikia na kupunguza au kuachana kabisa na matumizi ya kuni na mkaa ambao upatikanaji wake ni mgumu, aghali na siyo rafiki kwa mazingira.

Mhandisi Saidy alisema REA imefanya tafiti kadhaa za majaribio kuhusu nishati ya kupikia mathalani mradi wa kutumia tungamotaka, ambapo mifumo husika ilipelekwa katika maeneo 725 yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post