WAZIRI AWESO: MRADI WA MAJI KIGAMBONI KAZI IFANYIKE USIKU NA MCHANA

 Waziri wa Maji, Juma Aweso amewataka wakandarasi wa mradi wa Maji wa Visima Kigamboni kuanza utaratibu wa kufanya kazi usiku na mchana ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu kazi ili mradi huu ukamilike kwa haraka sana mwezi ujao.


Pamoja na hilo amesema licha ya kuwa hali ya upatikanaji wa maji bado haijakaa sawa, wamedhibiti baadhi ya maeneo ambayo maji yalikuwa yakichepushwa na kusababisha upungufu wa maji.

Amewaelekeza DAWASA kipindi hiki kuhakikisha wanaendelea na jitihada za kukabiliana na hali ya upungufu wa Maji ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mgao kwa uwazi ili wananchi waweze kupata na kuhifadhi Maji.

Waziri Aweso ameyasema hayo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa tanki la maji Kigamboni Kimbiji jijini Dar es Salaam uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 80 ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 15 za maji zitakazosaidia Kaya za Kigamboni na maeneo mengine ya Dar Es Salaam.

Waziri Aweso amewataka wakazi wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mpito cha uhaba wa upatikanaji maji wakati serikali ikiendelea na jitihada za kuweka sawa tatizo hilo.

Kwa upande wake , Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Fatma Nyangasa ameitaka Kampuni ya Advent ambayo ndio wakandarasi wa mradi huo, kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na kuwa uongozi wa wilaya utahakikisha unasimamia ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kuasaidia wakazi wa Kigamboni ipasavyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post