MKUU WA MKOA KATAVI ASISITIZA ELIMU YA KODI IWE ENDELEVU KWA WAFANYABIASHARA

 

 Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko akiongea na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuanza kufanya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango kwa wafanyabiashara mkoani hapo.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), waliomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuanza kufanya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango kwa wafanyabiashara mkoani hapo.

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha kwamba elimu ya kodi iliyoanza kutolewa mkoani hapo iwe endelevu kwa wafanyabiashara ili wapate elimu ya kutosha itakayowawezesha kulipa kodi zao stahiki na kwa wakati.

Kauli hiyo ameitoa leo ofisini kwake wakati alipokutana na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliopo mkoani Katavi kwa ajili ya kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi ya mlango kwa mlango, ambapo amesema kuwa, baadhi ya wafanyabiashara hawajapata elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya kodi na wengine hawajui kwanini wanalipa kodi.

“Nachoamini mimi ni kwamba, nia yetu kubwa ni kuvuka lengo, pamoja tumefikia asilimia nzuri lakini wako watu ambao hawajafikiwa na hawana elimu ya kutosha kuhusu kodi, wengine wanaona kwamba kutoa kodi ni kama manyanyaso, kwahiyo tunapaswa tutoe elimu endelevu katika mkoa wa Katavi ili waelewe kwanini wanalipa kodi na waweze kulipa kodi stahiki kwa hiari”, alisema Mrindoko.

Ameongeza kuwa kuna katika mkoa wake amebaini changamoto ya matumizi hafifu ya mashine za kodi za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) na baadhi ya walipakodi wamekua wakikiuka matumizi yake kutokana na kutokujua hali inayopelekea ukwepaji mkubwa wa kodi, hivyo ameitaka pia TRA kuwaelimisha walipakodi kuhusu umuhimu wa matumizi yam ashine za EFD ili wafanyabiashara waitikie wito wa kutoa risiti kikamilifu.

Aidha, amebainisha kuwa mkoa wake una fursa nyingi mbalimbali za kibiashara hususani katika kilimo cha mazao mbalimbali, mifugo, madini pamoja na viwanda vidogo vidogo, hivyo amekitaka kikosi kazi cha utoaji elimu kilichopo mkoani hapo kutoa elimu ya kutosha kwa makundi hayo bila kuwasahau wajasiriamali.

Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoani Katavi, Bw. Jacob Mtemang’ombe amesema kampeni ya utoaji elimu kwa walipakodi itawagusa wafanyabiashara wa maeneo yote ya Mkoa wa Katavi ili kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wafanyabiashara mkoani hapo ikiwemo namna wanavyofuata sharia za kodi.

“Katika zoezi hili tunatarajia kuwafikia wafanyabiashara wa maeneo mengi ikiwemo Mpanda mjini, Kasekese, Karema, Majimoto, Inyonga, Mlele na maeneo mengine na tutatoa elimu hii mlango kwa mlango ili tusikie changamoto za wafanyabiashara na kuzitatua. Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote kutoa ushirikiano kwa waelimishaji kutoka TRA watakaopita madukani ili kwa pamoja tuweze kufikia lengo la kampeni hii”, alisema Mtemang’ombe.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wamepongeza kupatiwa elimu ya kodi na watu wa TRA na pia wameweza kuwasilisha kero zao za kikodi hususani kuhusu makadirio, elimu kuhusu mashine za EFD na kuiomba pia TRA kuwaelimisha wateja kujenga tabia ya kudai risiti wanaponunua bidhaa dukani ili kuwaepusha wauzaji wasipate adhabu zinazotokana na kutodai risiti hizo.

Kampeni ya elimu kwa Mlipakodi kwa sasa ipo mkoani Katavi ikiwa na lengo la kuhakikisha kwamba wafanyabiashara mkoani hapo wanapatiwa elimu ya kodi na wanalipa kodi zao stahiki na kwa wakati.

Post a Comment

Previous Post Next Post