Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akijibu swali la Mbunge wa Meatu, Mhe.Leah Jeremiah Komanya ambapo amesema Serikali itaendelea kutenga fedha za ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo magari ili kukabiriana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu.
………………………………………………………………..
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja amesema Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kujenga uwezo wa Halmashauri kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Mhe. Mary Masanja ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati wa akijibu maswali ya wabunge kuhusu hatua na mikakati mbalimbali inayoendelea kuchukuliwa na Wizara kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu akibainisha kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (TAWA) imeongeza watumishi 87 sawa na ongezeko la asilimia 40 ili kuimarisha usimamizi wa maeneo ya mapori ya akiba katika wilaya za Meatu na Itilima.
Aidha, amesema Wizara itaendelea kuimarisha na kuendeleza tafiti na kutumia mbinu mbalimbali za udhibiti na ufuatiliaji wa makundi ya tembo ikiwemo kuwafunga mikanda maalum ya kielektroniki ya kufuatilia mienendo ya makundi korofi ya tembo, kufundisha na kuviwezesha vikundi vya wananchi kufuatilia maeneo walipo tembo, matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani, kutengeneza minara ya kuangalia mbali, matumizi ya mizinga ya nyuki na vifaa vyenye mwanga mkali pamoja na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapovamiwa na wanyamapori hao