Akiwasilisha bejeti hiyo Waziri Aweso ameeleza mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya maji katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Machi, 2021 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa huduma za maji nchini kutoka asilimia 70.1 vijijini na 84 mijini mwaka 2019/20 hadi asilimia 72.3 vijijini na 86 mijini.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya maabara za ubora wa maji zenye ithibati kutoka moja ya Mwanza hadi kufikia saba, kuzinduliwa kwa miradi mikubwa ya maji ya Tabora – Igunga - Nzega pamoja na Isaka Kagongwa baada ya utekelezaji kukamilika. Aidha kukamilika kwa utekelezaji wa kihistoria wa miradi 422 ya maji ambapo kati ya hiyo ya vijijini ni miradi 355 na mijini miradi 67.
Waziri Aweso amesema hivi sasa kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi ya maji imeongezeka na gharama za ujenzi zimepungua kutokana na kutumia utaratibu wa force account.
Mafanikio mengine ni pamoja na kuanza kutoa huduma ya maji kwa miradi 85 iliyokuwa na changamoto baada ya kufanya mabadiliko makubwa katika utaratibu wa usimamizi.