Waziri Wa Maji Aitaka EWURA Kuhakikisha Mamlaka Za Maji Zinaboresha Huduma

 

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, jana Aprili 28,2021 amefanya kikao kazi na watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Katika Kikao hicho Waziri ameitaka EWURA wahakikishe mamlaka zote za maji nchini, zinatoa ankara sahihi kwa wateja wa maji na zinafuata sheria katika utoaji wa huduma za maji na kwamba Mwananchi yoyote asikatiwe maji kuanzia siku ya ijumaa mchana, siku za mwisho wa wiki na siku za sikukuu.

"Siku za mwisho wa wiki na zile za sikukuu ofisi zote zimefungwa je mnataka huyu mwananchi akalipie wapi?" aliuliza.

Kuhusu ubovu wa miundombinu na upotevu wa maji, Waziri Aweso ameitaka EWURA kuhakikisha mamlaka za maji zinaboresha miundombinu na kudhibiti maji yanayopotea njiani bila kumfikia mtumiaji wa mwisho.

"Suala la kelele za upotevu wa maji lifike mwisho na mamlaka za maji zitakazo fanya vibaya katika hili zichukuliwe hatua", Alisema

Akizungumzia kuhusu wateja sugu wasiolipia ankara za maji, Mhe. Aweso aliitaka EWURA iongeze nguvu katika kutoa elimu kwa umma.

"Ni haki ya Mwananchi kupatiwa huduma ya maji, pia asisahau ana wajibu wa kulipia maji hayo, mwananchi apewe elimu ili aone fahari kulipia huduma na asibambikiwe bili wala kutozwa huduma ambazo hazijapitishwa na EWURA.

Mhe.Aweso amemalizia kwa kutoa pongezi kwa EWURA kwa utendaji mzuri na kuwataka wafanyakazi wawe na ushirikiano na kufanya kazi kwa umoja ili kufikia lengo la uwepo wa taasisi hiyo nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post