WAITARA AITAKA TRC KUTOA HUDUMA BORA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akimsikiliza Meneja Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Sehemu ya Morogoro hadi Dar es Salaam, Mhandisi Simon Mmbaga, akimweleza hatua ya ujenzi wa Jengo la abiria katika stesheni ya Morogoro, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa reli hiyo, mwishoni mwa wiki, mkoani Morogoro. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa

Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya utandikaji wa reli ya Kisasa ya SGR katika stesheni ya Morogoro, Sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (kulia), akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha Stesheni ya Morogoro, wakati Naibu Waziri huyo alipokagua ujenzi wa kituo hicho, mwishoni mwa wiki, Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akiangalia hatua iliyofikiwa ya utandikaji reli ya kisasa ya SGR, katika stesheni ya Morogoro, alipokagua maendeleo ya ujenzi wake, mwishoni mwa wiki, mkoani Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, kuhusu hatua ya ujenzi wa Jengo la abiria katika stesheni ya Dar es Salaam Morogoro wakati Naibu Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa reli stesheni, mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salam.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (kulia), akitoa malekezo kwa Mhandisi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Morogoro, Blasius Mwita, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Stesheni ya Morogoro, mwishoni mwa wiki, Mkoani Morogoro. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (wa pili kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Wataalam wa Kampuni ya Yapi Merkezi, mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Stesheni ya reli ya Kisasa ya SGR, jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. 

PICHA NA WUU

********************************

Serikali imelitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuhakikisha linatoa huduma bora na za viwango kwa Watanzania mara baada ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kukamilika na kuanza kutoa huduma ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mheshimiwa Mwita Waitara,  kufuatia wasiwasi wa wananchi kuhusu masuala ya miundombinu ya umeme wa reli hiyo ambapo pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali kupitia Shirika hilo imejidhatiti kwa kuweka vyanzo vya umeme vitatu tofuati na vichwa vya kutumia dizeli ili kutatua changamoto zozote zitakazojitokeza.

“Napenda kuwatoa wasiwasi Watanzania kuwa Serikali kupitia TRC imejipanga sawasawa kuhakikisha umeme hautakuwa changamoto wakati wa uendeshaji wa treni hii” amesisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Waitara amelitaka Shirika hilo kujipanga na kuhakikisha kuwa wataalam wazawa waliopata ujuzi kwenye mradi huo wanatumika ipasavyo mara baada ya mradi kukamilika.

Waitara, amelipongeza Shirika hilo kwa kuajiri watalaam na kusimamia vizuri mradi huo kwa Sehemu ya Makutupora hadi Morogoro na Morogoro hadi Dar es Salaam.

Naibu Waziri Waitara amamhakikishia Mkurugenzi wa TRC kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa fedha ili mradi uweze kukamilika na Watanzania wafaidi matunda ya Serikali yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Masanja Kadogosa, amesema kuwa TRC imeshaajiri wahandisi zaidi ya 200 ambao kwa sasa wamewekwa kwenye miradi ili kupata ujuzi na uendeshaji wa reli hiyo ya kisasa mradi utakapokamilika.

Kuhusu upatikanaji wa mabehewa Kadogosa amefafanua kuwa tayari manunuzi yako kwenye hatua nzuri na vichwa vitawasili mapema mwezi Julai na majaribio ya treni ya kwanza kwa sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro yatafanyika mwezi Agosti.

Naye, Meneja Mradi wa sehemu ya Morogoro – Dar es Salaam, Mhandisi Simon Mmbaga, amesema mradi huo kwa sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro umeshakamilika na asilimia zaidi ya 93 na kazi zinazoendelea kukamilishwa ni pamoja na kuunganisha mifumo mbalimbali katika vituo.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amekamilisha ziara yake ya siku mbili ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi wa reli ya Kisasa ya SGR kwa sehemu ya Makutupora hadi Morogoro na Morogoro hadi Dar es Salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post