WAITARA AAHIDI KUDILI NA WAKANDARASI NA WAFANYAKAZI WABABAISHAJI

 Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara akisisitiza jambo kwa  menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya  Mfuko wa Barabara (hawapo pichani),  wakati alipotembelea na kufanya  nao  kikao kazi kilichofanyika katika ofisi za bodi hiyo, jijini Dodoma

Meneja wa Mfuko wa  Barabara, Bw. Eliud Nyauhenga, akiwasilisha taarifa kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha kilichofanyika katika ofisi ya Bodi, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, (mbele wa kwanza kulia), akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti na wafanyakazi wa  Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), mara baada ya kumaliza kikao kazi kilichofanyika Jijini Dodoma.

*******************

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewaonya wakandarasi na wafanyakazi wababaishaji na wanaoidanganya Serikali kuwa wana sifa na vigezo lakini wanajenga barabara na madaraja chini ya viwango  kuacha tabia hiyo mara moja.

Amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja chini ya viwango  husababisha gharama kubwa kwa Serikali kutokana na kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara.

Naibu Waziri Mwita ametoa kauli hiyo jijini Dodoma, katika kikao kazi na menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na kupokea taarifa ya Bodi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine ameupongeza mfuko huo kwa namna unavyoweza kusimamia matengenezo ya barabara nchi nzima kwa uharaka unaoendelea kufanywa na Wakala wa Barabara  (TANROADS) pamoja na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). 

Amezungumzia umuhimu wa wafanyakazi kutoa elimu sahihi kwa Jamie ili kuilinda  miundombinu yote ya Barabara, Madaraja, Reli, Bandari, Vivuko na Viwanja vya Ndege ili idumu kwa muda mrefu.

“Tutahakikisha tunachujana humu humu ndani na ukigundua kuwa wewe sio mwenzetu ujitafakari mapema kabla sijakufikia, tunahitaji watumishi wazalendo na wakandarasi wenye sifa na weledi sio wababaishaji”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 
Waitara amewataka watendaji kuongeza kasi katika maamuzi hasa pale inapotokea dharura ya madaraja na barabara kukatika na kusababisha wananchi kukosa huduma mbalimbali za kijamii. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa watumishi kutumia muda wao wa Serikali vizuri kwa kuleta michango chanya yenye ubunifu pamoja na kuweka mkazo katika kutatua changamoto za wananchi kwa haraka na kasi.

 Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bodi hiyo kwa Naibu Waziri huyo, Meneja wa Mfuko wa Barabara Bw. Eliud Nyauhenga, amesema kuwa mfuko umeweza kufadhili tafiti mbalimbali zinazofanywa kwenye ujenzi wa gharama nafuu ili kujenga barabara nyingi zaidi na imara. 

Nyauhenga, ameongeza kuwa Bodi imeendelea kutoa elimu kwenye ngazi zote kuhusu matumizi bora ya barabara ili kuilinda miundombinu hiyo na kupunguza gharama kubwa za matengenezo.

Naibu Waziri Waitara yupo katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Tanga yenye lengo la kujitambulisha, kuzifahamu taasisi zinazosimamiwa na Wizara yake, kukagua miradi pamoja na kuzungumza na wafanyakazi kuhusu mwelekeo wa Serikali.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post