Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Abbas Kayanda (aliyesimama) akifungua kikao cha Ujirani mwema kati ya Watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Viongozi wa Wilaya ya Karatu, Kulia kwake ni Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Audax Bahweitima na Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Waziri Mourice.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA anayesimamia huduma za Shirika Bw. Audax Bahweitima akielezea namna NCAA inavyoshirikiana na Wilaya ya karatu kupitia kata zinazozunguka hifadhi hiyo kutekeleza program za ulinzi shirikishi.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Abbas Kayanda akizungumza na washiriki wa mkutano wa ujirani mwema uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Karatu Bw. Waziri Mourice akizungumza katika kikao cha ujirani mwema kati ya NCAA na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii Mdala Fedes akielezea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii kwa Wananchi wa Karatu kupitia program ya ujirani mwema.
Sehemu ya Watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakisikiliza hoja za wadau wakati wa kikao cha ujirani mwema kilichofanyika Wilayani Karatu Mkoani Arusha.
********************************
Na Kassim Nyaki NCAA
Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) umefanya kikao cha Ujirani mwema na Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa lengo la kuimarisha mahusiano na uimarishaji wa Uhifadhi Shirikishi kwa wananchi wa vijiji vya Wilaya hiyo vinavyozunguka Hifadhi ya Ngorongoro.
Akifungua kikao cha Ujirani mwema Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Abbas Kayanda ameishukuru NCAA kwa kuandaa kikao hicho Muhimu na kusisitiza kuwa programu za ujirani mwema ziwe endelevu ili kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wa vijiji vya Karatu vinavyozunguka Hifadhi hiyo kujiepusha na viashiria vya vitendo vya ujangili hasa kwa Wanyama wanaotoka ndani ya Hifadhi na kuingia kwenye mashamba ya wananchi yaliyopo jirani na Hifadhi hiyo.
“Pamoja na program mbalimbali za ujirani mwema najua kuna changamoto ya Wanyamapori kuvamia mashamba ya wananchi lakini nawasihi Viongozi wa kata za Eyasi, Oldeani, Ganako, Rhotia na Mbulumbulu ambazo zinapakana na Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kushirikiana na NCAA kuwaelimisha wananchi kuona Hifadhi hii ni yao na watoe ushirikiano wa kutosha kwa viashiria vyovyote vya uhalifu kwa Wanyama wanapoingia katika maeneo yao” amesisitiza Mhe. Kayanda.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA (Huduma za Shirika) Bw. Audax Bahweitima ameeleza kuwa kupitia dhana ya uhifadhi shirikishi NCAA imepata faida mbalimbali kwa Vijiji vinavyopakana na Hifadhi hiyo ya ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi shirikishi kwenye eneo la Hifadhi, uelewa wa Jamii kuheshimu sheria za Uhifadhi, Wananchi kufichua wahalifu wa uwindaji wa Wanyamapori, Kukuza uelewa wa jamii katika athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira, Kukuza uelewa wa jamii katika faida za uhifadhi katika kuchangia miradi ya maendeleo, Ustawi wa wanyamapori na misitu ambayo ni faida kwa Taifa na jamii katika uchumi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa NCAA anayesimamia Maendeleo ya Jamii Fedes Mdalla ameeleza kuwa katika kusaidia na kuendeleza shughuli za Ujirani Mwema Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka 5 iliyopita imechangia jumla ya Shilingi 783,000,000 kwa baadhi ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya kijamii, miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu Milioni ambapo NCAA ilichangia milioni 600,000,000, ujenzi wa jengo la Shule ya Sekondari Welwel Shilingi Milioni 53,000,000, ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Silahamo milioni 120,000,000 na mradi wa maji Kijiji cha Mang’ola juu Shilingi 10,000,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Karatu Bw. Waziri Mourice ameeleza kuwa kupitia programu ya Ujirani mwema NCAA imeisaidia halmashauri yake kutekeleza program mbalimbali ikiwemo, Kutoa elimu ya kukuza uelewa kuhusiana na faida zitokanazo na utunzaji wa hifadhi na mazingira kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari, utoaji wa ajira za muda kwa vijana wa Karatu, kuwezesha uundwaji na kusaidia vikundi vya ufugaji nyuki na vikao vya ujirani mwema kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi.
Bw. Waziri ameishauri Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendeleza utaratibu wa vikao vya ujirani mwema ili kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza hasa za Wanyamapori kuingia kwenye mashamba ya wananchi na kuwadhuru na kuelimisha wananchi kutovamia korido za wanyama