Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi uliofanyika kwa njia ya Mtandao (Video Conference) leo tarehe 8 Aprili 2021.
……………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
NCHI 19 za Umoja wa Uzalishaji wa Almasi Barani Afrika (ADPA) zimekubaliana kuongeza Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za mawasiliano katika jumuiya hiyo.
Hayo yamebainishwa leo April 8,2021 na Waziri wa Madini, Dotto Biteko,wakati wa mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi za Afrika zinazozalisha madini ya Almasi ambao umefanyika Jijini Dodoma kwa njia ya Mtandao (Video Conference).
“Kiswahili kitakuwa moja ya lugha ya mawasiliano katika umoja huu, awali kulikuwa na Kifaransa na Kiingereza na Kireno,” alisema.
Biteko amesema kuwa hadi sasa Jumuiya iliyoanza mwaka 2006, zilikuwa lugha tatu za Kifaransa, Kiingereza na Kireno.
Pia mkutano huo walikubaliana ndani ya miezi sita kamati tendaji ya ADPA itafanya marekebisho na maboresho katika mfumo wa menejimenti ya utendaji ya umoja huo.
Mhe.Biteko amesema kuwa pia Tanzania imezialika nchi wanachama na kufanya ukaribisho wa kutumia soko la madini hayo nchini kuuza madini yao na tutaendelea kusukuma mbele jambo hilo.
“Tumeoa ukaribisho wa kutumia soko la almasi, tumenifanya na tutaendelea kulisukuma mbele kwa sababu tutakuwa wenyeviti wa ADPA,” amesema
Biteko amesema kuwa wakati Tanzania itakuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, makamu mwenyekiti wa ADPA atakuwa nchi ya Zimbabwe ambaye atashika madaraka ya uenyekiti baada ya Tanzania kumaliza muda wake.
Zimbabwe itapokea kijiti cha kuongoza jumuiya hiyo baada ya Tanzania ili kusukuma mbele maendeleo ya jumuiya hiyo.
Naye, Waziri wa Madini na Nishati wa Jamhuri ya Namibia, Tom Alweendo wa nchi ambayo imemaliza uenyekiti wake, ameitaka Jumuiya hiyo kupata viongozi shupavu wa Kamati Tendaji watakaosaidia kuweka msukumo katika utekelezaji wa malengo ya jumuiya hiyo.
Ameongeza kuwa, kama wanachama ni lazima wachochee na kuweka mikakati ya kupigania maslahi ya Afrika kwa madini ya Almasi ikiwemo kuzitaka nchi hizo kuhakikisha zinalipa michango yao kwa mujibu wa sheria.
Pia, Ametumia fursa hiyo kuelezea yale ambayo yalifanywa na nchi hiyo wakati ikishikilia kiti cha Uenyekiti na kueleza kuwa, pamoja na kipindi chake kukabiliwa na changamoto za janga la ugonjwa wa Corona, ilifanikiwa kuunda kamati ya uendeshaji ya jumuiya hiyo.
Mkutano wa 7 wa Mawaziri wa Nchi zinazozalisha madini ya Almasi Afrika, umehudhuriwa na nchi zote 19 wanachama wa umoja huo zikiwemo Nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea na Sierra Leone. Mbali na hizo, Nchi waangalizi zilizoshiriki ni Algeria, Jamhuri ya Congo, Cote D’ivore, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania pia zimeshiriki.