WIZARA MPYA TUCHAPE KAZI KWA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

 Prisca Ulomi, WMTH

 
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka watumishi wa Wizara yake pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi ya Serikali ya Awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan
 
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati akifungua mkutano namba 2/2020/2021 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma
 
Amewaeleza wafanyakazi wa Wizara hiyo kuwa wameyasikia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara yetu ikiwemo usimamizi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), mikakati ya kufikisha mawasiliano kwenye maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu na kuangalia upya suala la mabando na kuweka uratibu mzuri wa utekelezaji wake pamoja na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ambapo tayari Wizara ilianza kuyatekeleza na kufanyia kazi hivyo ana imani kuwa wataalamu wa Wizara wana majibu yote na ndio umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano
 
Vile vile, amesisitiza kwa wafanyakazi hao kuwa Wizara hii sio ya kwake wala ya menejimenti ya Wizara hiyo bali ni Wizara ya wafanyakazi wote, hivyo wafanyakazi wote wana wajibu wa kutumikia watanzania kuendana na majukumu ya kila mfanyakazi kwa kuongeza kasi zaidi ya kutekeleza majukumu ya Wizara ikizingatiwa kuwa Wizara imeongezewa bajeti kutoka shilingi bilioni kumi na sita kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 na kufikia shilingi bilioni 216 kwa mwaka wa fedha wa 2021/22.
 
Pia, amewataka wafanyakazi kuhakikishia wanaongeza kasi ya kuitambulisha Wizara mpya kwa wananchi ili waelewe majukumu ya Wizara kwa kuzingatia kuwa Wizara hii ndiyo yenye dhamana ya masuala ya TEHAMA nchi nzima na inasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA na Wizara hii ni mtambuka, ni kiungo mchezeshaji kwa kuwa inagusa nyanja ya kijamii, kiuchumi, ulinzi na usalama
 
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Andrea Mathew amewaeleza wafanyakazi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita ni sawa na makocha wa mpira, hivyo kila mmoja awajibike kutekeleza majukumu yake na kuonesha anatosha katika nafasi yake na kuendeleza ushirikiano baina ya wafanyakazi na viongozi ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake kuendana na matakwa ya Serikali ya sasa
 
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa lengo la Mkutano huo ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 na kuwasilisha mpango wa bajeti kwa mwaka 2021/22; mada mbali mbali zinazohusu afya na ustawi wa wafanyakazi mahali pa kazi na kuhimiza viongozi kuzingatia maslahi ya wafanyakazi na kuleta umoja, mshikamano na upendo kazini.
 
Mwenyekiti wa TUGHE wa tawi la Mawasiliano, Laurencia Masigo, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo, amewashukuru viongozi wa Wizara kwa kuchochea amani mahali pa kazi na kuwaomba viongozi kufuatilia mwongozo wa gharama za usafiri wa mabasi kutoka kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Usafiri Nchi Kavu (LATRA) ili watumishi waweze kulipwa nauli stahiki wakati wa likizo zao na kufuatilia malipo ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi kwa mamlaka husika ili watumishi 19 waliobaki kati ya watumishi 30 waweze kulipwa.
 


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile(wa pili kulia) akifungua baraza la wafanyakazi la Wizara hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Kulia ni Naibu wake Mhandisi Kundo Mathew, wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi. 

Viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiimba wimbo wa mshikamano daima wakati wa Mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma, kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi, akifuatiwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Zainab Chaula, akifuatiwa na Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile na Mwisho ni Naibu wake, Mhandisi Kundo Mathew
Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Wizara ya Mawasiliano Teknolojia ya Habari Laurencia Masigo
akizungumza katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Kulia ni ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula (kulia) akizungumza katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.katikati ni Naibu wake Dkt. Jim Yonazi na Kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE tawi la Wizara ya Mawasiliano Laurencia Masigo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akizungumza katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma. Wa pili kulia ni Waziri wake Dkt. Faustine Ndugulile akifuatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula na kushoto ni Naibu wake Dkt. Jim Yonazi
Viongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakipokea zawadi za pongezi kutoka kwa menejimenti ya Wizara hiyo kwa kuaminiwa na Mhe. Rais kuendelea kuongoza Wizara hiyo



Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akisalimiana na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Laurensia Masigo (kushoto) katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa  Wizara hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma wa Pili kulia ni Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile akifuatiwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Zainab Chaula akifuatiwa na Naibu wake Dkt. Jim Yonazi

Baadhi ya wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakimsikiliza Waziri wa Wizara hiyo (hayupo pichani) wakati akifungua baraza hilo lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, Dodoma.

Post a Comment

Previous Post Next Post