Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale, wakati akikagua barabara ya mchepuko wa Kusini, maarufu kama Arusha Bypass (Kilometa 42.4). Wengine ni watumishi wa TANROADS mkoa wa Arusha.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale, akielezea jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akikagua barabara ya mchepuko wa Kusini, maarufu kama Arusha Bypass (Kilometa 42.4). Wengine ni watumishi wa TANROADS mkoa wa Arusha.
Mhandisi wa Miradi Colman Ramadhani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dodoma, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, katika eneo la Dosidosi, barabara ya Kongwa kwenda Kibaya hadi Arusha (kilometa 430).
Picha na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
*************************************
Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Arusha, imekamilisha miradi ya kitaifa ya ujenzi wa barabara za Sakina hadi Tengeru (njia nne) Kilometa 14.1, barabara ya mchepuko wa Kusini (Arusha Bypass) Kilometa 42.4 pamoja na ujenzi wa barabara ya Kia hadi Mererani Kilometa 26. Barabara zote hizi zimejengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika kwa asilimia mia moja.
Akiongea na watumishi wa TANROADS mkoa wa Arusha, mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua barabara hizo Naibu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya aliwapongeza watumishi hao kwa kusimamia vyema miradi ya ujenzi wa barabara hizo na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi wake, lakini pia kwa kuhakikisha barabara zote wanazozisimamia ndani ya mkoa wa Arusha zinapitika katika majira yote ya mwaka.
“Nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara iliyopo, lakini pia miradi mipya itakayotengewa fedha kwenye bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, nayo itatekelezwa”. Alisema Kasekenya
Nae Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha Mhandisi Johnny Kalupale, alimuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa ujenzi wa barabara ya Sakina hadi Tengeru (njia nne), yenye urefu wa kilometa 14.1 umegharimu shilingi bilioni 70.365, barabara ya mchepuko wa kusini (kilometa 42.4) shilingi bilioni 86.778 na barabara ya Kia hadi Mererani (kilometa 26) shilingi bilioni 32.
Aliongeza kuwa kwa sasa TANROADS mkoa wa Arusha inaendelea na usimamizi wa miradi ya ujenzi wa barabara za Mto wa Mbu hadi Loliondo (kilometa 49), Kijenge hadi Usariver (kilometa 20), ujenzi wa mzani wa kisasa wa kupima magari katika eneo la Kimokouwa barabara ya Namanga pamoja na kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Sakina hadi Tengeru (kilometa 9.3).
Naibu Waziri Kasekenya alikuwa katika ziara ya siku moja mkoani Arusha akitokea Dodoma kupitia barabara ya vumbi ya Kongwa kwenda Kibaya hadi Arusha (kilometa 430), ambapo kwa sasa usanifu wa barabara hiyo umekamilika na ujenzi wake utatangazwa mara baada ya kutengewa fedha katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi