TMDA: KUWA MAKINI UNAPONUNUA KONDOM KWA SABABU UNAENDA KUITUMIA MWILINI MWAKO

 

Mtaalamu wa Uchunguzi katika Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika mkoa wa Dar es salaam Bw. Saxson Mwambene akitoa maelezo kwa waandishi wa habari waliofanya ziara ya kimafunzo katika maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) iliyoko Mabibo Mkoani Dar es salaam,  kulia ni Happyness Seswa Mchunguzi wa Maabara.

Happyness Seswa Mchunguzi wa Maabara akiwalelezea waandishi wa habari namna uchuguzi wa ubora wa kondom unavyofanyika katika maabara hiyo.

Happyness Seswa Mchunguzi wa Maabara akipima uimara wa kondom mbele ya  waandishi wa habari waliotembelea maabara hiyo kwalengo lakujifunza namna maabara hiyo inavyofanya kazi.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma,wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),Gaudensia Simwanza akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa ziara hiyo.

Mtaalamu wa Uchunguzi katika Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika mkoa wa Dar es salaam Bw. Saxson Mwambene akiwafafanulia jambo waandishi wa habari waliotmbelea maabara hiyo.

Baadhi ya waandishi wa habari wakiingia kwenye maabara ya TMDA wakati walipotembelea maabara hiyo.

………………………………………..

Mtaalamu wa Uchunguzi katika Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika mkoa wa Dar es salaam Bw. Saxson Mwambene ameeleza namna maabara hiyo inavyofanya kazi ili kuhakikisha vifaa tiba vinavyofanyiwa uchunguzi katika maabara hiyo vinakuwa bora kwa matumizi ya binadamu.

Mwambene ameeleza hayo mbele ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wanaofanya ziara ya siku tatu ya mafunzo katika maabara hiyo iliyoko Mabibo katika manispaa ya ubungo mkoani Dar es salaam ambapo leo ilikuwa ziara maalum kujifunza kuhusu uchunguzi wa ubora  Kondom

Amesema katika suala la kondom wanachunguza matundu madogo madogo yanayoweza kutokea wakati wa uzalishaji, wanachunguza vifungashio kwa sababu vikitoboka na kupitisha hewa Kondom haiwezi kuwa na ubora tena hii ni kutokana na kilainishi chake kinatoka na kikitoka oksijeni inaingia kondom inapoteza ubora wake wakati wa matumizi.

“Kwa kifupi maana yake ni kwamba Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inachunguza ubora wa Bidhaa ya Kondom tangia inapoingia bandarini, Inapohifadhiwa na kwenye Maduka yenyewe kwa kutumia mashine zetu mbalimbali ikiwemo hii inayoitwa  inayoitwa (AUTOMATED INFLATION SYSTEM),” amesema Mwambene.

Mwambene ameongeza kuwa kwenye maduka wanawatumia wakaguzi wao katika maeneo mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya ukaguzi ili kuhakikisha bidhaa yoyote ambayo iko chini ya kiwango haiingii sokoni.

 Amesema zipo mashine mbalimbali zinazofanya kazi ya uchunguzi wa Kondom kama vile Mashine ya kuchunguza mashimo madogomadogo ya Kondomu  (Electric Leak Tester For Condom),  Mashine ya kupima ukubwa wa Kondom (Automated Width Tester) , Mashine ya kuangalia ubora wa vifungashio (Automated Wet Package Seal Integrity Tester For Condom), Mashine ya kupima ubora wa Gloves na Komdomu za Kike (Visual Leak Tester For Gloves/Condom), Mashine ya kupima uimara na ubora wa Kondom (Automated Inflation System).

Ameongeza kuwa TMDA imekuwa ikipokea bidhaa mbalimbali za kondom na wanapofanyia uchunguzi nyingi zinakuwa na ubora kwa matumizi na mara chache zinatokea bidhaa ambazo hazina viwango na inapotokea bidhaa kama hiyo tunachukua hatua mara moja kuhakikisha haziingii sokoni. 

Amewaonya wananchi kuhakikisha wanakuwa makini wakati wanapokwenda kununua kondom madukani: “Ni muhimu kuangalia unanunua kondom kwenye duka la namna gani na kabla ya kununua angalia muda wake wa matumizi (Expire Date) kama umekwisha au bado ili usiingie kwenye matatizo kwa sababu kondom utakayonunua unakwenda kuitumia kwenye mwili wako ni lazima kuwa makini na afya yako.” 

Aidha Mtaalamu huyo ameongeza kuwa kazi wanayoifanya ya kupima ubora wa bidhaa hiyo ni kazi ya kisayansi hivyo wanajukumu la kufanyakazi kazi hiyo kwa umakini mkubwa na uadilifu kwani jamii ya watanzania ina imani kubwa na (TMDA) katika kuchunguza na kuthibitisha bidhaa zote za vifaa Tiba na Dawa kabla hazijawafikia walaji ambao ni wananchi.

Katika uchunguzi wetu tunatumia Sayansi lazima tuiheshimu hapa tukikosea au mmoja wetu akachukua rushwa atakuwa ameikosea Familia yake na  Jamii nzima ya Watanzania hivyo tunafanyakazi kwa umakini mkubwa na kufuata miongozo na maadili ya kazi” amesema Mwambene.

Naye Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma,wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),Gaudensia Simwanza amesema ziara hiyo ya mafunzo itafanyika kwa siku tatu ambapo itasaidia kuwaongezea uelewa waandishi wa habari na kujua umuhimu wa Maabara za uchunguzi wa Dawa na Vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kazi za Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMAD).

Post a Comment

Previous Post Next Post