Wafanyakazi wanawake Shirika la Taifa la Madini STAMICO wakisherekea Siku ya wanawake Duniani ofisini kwao.
SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) leo tarehe 8 Feb 2021 imeungana na wanawake wote Duniani kusheherekea siku ya wanawake kupitia kauli mbiu ya “Wanawake Katika Uongozi, Chachu Kufikia Dunia yenye Usawa” yenye lengo la kuhamasisha usawa na uwajibikaji hasa katika nafasi za uongozi.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugezi Mtendaji wa STAMICO Bw. Deusdedith Magala amewapongeza wafanyakazi wanawake kwa ubunifu na jitihada wanazozifanya katika utendaji kazi kwani wamekuwa na mchango mkubwa sana kwa Shirika.
“Mmekuwa wafanyakazi Hodari mnaoweza kufanya kazi katika mazingira yoyote, ukizingatia kazi za madini zina changamoto zake na kwa kuwa nyingi hufanyika mbali na maeneo ya mjini jambo linalopelekea kukaa mbali na familia zenu. Nawapongeza sana endeleeni kuchapa kazi kwa bidii”
Katika kusheherekea sikukuu hiyo wafanyakazi wanaume wa STAMICO nao wameamua kushikilia kwa muda majukumu ambayo yanashikiliwa na wafanyakazi wanawake ili kuwaruhusu wanawake hawa kwenda kushiriki ipasavyo katika maadhimisha ya siku ya sherehe hiyo.
Akiongea mmoja wa wafanyakazi wanaume, Afisa Masoko Mwandamizi Bw. Bilton Otto Alikuwa na haya ya kusema, “leo tumeamua kushikilia kwa muda majukumu ya wanawake ili kuwaunga mkono katika sikukuu yao hii muhimu. Ni furaha kwetu kuona wanawake wengi wanajitokeza kwa ujasiri kufanya kazi katika sekta ya madini”.
Aidha wafanyakazi wanawake wameushukuru na kufurahia ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi wa STAMICO jambo linalowarahisishia utendaji kazi na kuwafanya wasione utofauti katika maeneo ya kazi.
STAMICO imekuwa ikishiriki katika maadhimisho haya kila mwaka ili kuleta hamasa kwa wanawake kujiunga katika biashara ya madini ili waweze kujikwamua kiuchumi.