BILIONI 1.6 ZATOLEWA KWA AJILI YA KUHUISHA CHUO CHA TAIFA CHA SUKARI – KATIBU MKUU KUSAYA

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti Dkt. Wilhelm Mafuru wakati wa kikao hicho na Wadau wa tasnia ya sukari leo tarehe 5 Machi, 2021 katika ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Mkurugeni wa Bodi ya Sukari Profesa Kenneth Bengesi akichangia mada kwenye mkutano wa Wadau wa tasnia ya sukari pembeni yake kushoto ni Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Tasnia ya Sukari (SIDTF) dkt. Nephat Mkula leo tarehe 5 Machi, 2021 katika ofiisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Wadau wa tasnia ya sukari kuanzia kulia ni Mwakilishi wa Wakulima wadogo wa miwa nchini Balozi Ahmadah Ngemela kutoka Missenyi mkoani Kagera, Guy Williams Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha sukari cha Kilombero na mwisho ni Degratias Lyatto Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Maendeleo ya Tasnia ya Sukari.

Gere Mlingwa Balozi Mstaafu na Mkulima mkubwa wa miwa akichangia mada katika mkutano huo wa Wadau wa tasnia ya sukari.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho cha Wadau akiongoza kikao hicho leo tarehe 5 Machi, 2021 katika ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Kilimo mwenye suti ya kijivu katikati akiwa pamoja na Wadau wa tasnia ya sukari baada ya kumalizika kwa mkutano wao.

***********************************************

Katika kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa sukari; Mfuko wa Maendeleo wa Tasnia ya Sukari (SIDTF) umeidhinisha jumla ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kugharamia huduma za mafunzo, uendeshaji wa shughuli za Chuo cha Taifa cha Sukari pamoja na ununuzi wa vifaa vya mafunzo na ukarabati wa majengo.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu; Wizara ya Kilimo  Gerald Kusaya wakati wa kikao chake na Wadau wa tasnia ya  sukari  ikiwemo Bodi ya Sukari, Wizara ya Kilimo, Wakulima wakubwa na wadogo wa miwa na Wazalishaji sukari katika ukumbi wa mikutano wa Wizara, Jijini Dodoma leo tarehe 5 Machi, 2021.

Katibu Mkuu Kusaya amesema ukosefu wa Wakufunzi, uchakavu wa vitendea kazi vya kuendesha mafunzo na kuchakaa kwa miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Sukari (National Sugarcane Institute – NSI) kulisababisha kusimama kwa utoaji wa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu Kusaya amesema kuwa juhudi za Serikali na Wadau wa tasnia ya sukari za kuimarisha Chuo cha Taifa cha Sukari zimeshaanza na kwamba zinaendelea kufanyika ili Chuo hicho kiwe bora na kinachotoa mafunzo ya kilimo cha miwa na uzalishaji sukari nchini.

“Chuo cha Taifa cha Sukari nchini ndiyo Chuo pekee cha Afrika Mashariki na Kati kitakachokuwa kikiandaa Wataalam wa teknolojia ya sukari na kinatariwa kurejea katika kutoa mafunzo Mwezi Septemba 2021 na tutarajie mabadiliko makubwa.” Amesisitiza Katibu Mkuu Kusaya.

Katibu Mkuu Kusaya ameongeza kuwa juhudi za Serikali na Wadau zimewezesha Chuo cha Taifa cha Sukari kupata kibali cha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa mafunzo kwa Ngazi ya Astashahada na Shahada ya kilimo cha miwa (Sugarcane technology) na uzalishaji wa sukari (Sugar technology).

Naye Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sukari Bwana Aloyce Kazimili  amesema kwa sasa tayari kuna Walimu ambao wanatoa mafunzo hayo lakini hawakusomea taaluma ya kilimo cha miwa kwa sababu hiyo  Walimu hao ni vyema wakasomeshwa na Serikali kwenye eneo hilo ili rahisi wao kuajiriwa mara kibali cha ajira kitakapotolewa.

Katibu Mkuu Kusaya amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Kilimo kuwapa uhamisho wa muda Watumishi wawili wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi na Mkaguzi wa Ndani ili irahisishe hatua za awali za kuhuisha uanzishwaji wa Chuo cha Taifa cha Sukari pamoja na mambo mengine amewahidi Wadau wa mkutano huo kuwa atahakikisha ukarabati unaanza mara moja kwa kutumia Wataalam wa ndani na kwa mvumo wa “force account”.

Post a Comment

Previous Post Next Post