BILIONI 137 KUBORESHA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI NCHINI

 



 Serikali kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) itapeleka Shilingi bilioni 137 katika Halmashauri  zote nchini kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari mwaka 2020/2021.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako mjini Kasulu wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa ya Darasa la nne, saba, kidato cha pili na cha nne lilofanyika wilayani Kasulu mkoani Kigoma


Waziri Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba inawekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kukabiliana na changamoto ya miundombinu  na kuwezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora na kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji.


"Kuna watu wamekuwa wakilalamika kuhusu changamoto za elimu, napenda kuwahakikishia kwamba Serikali ipo kazini kupambana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu," na hapa Kasulu nafurahi kuwa katika uandikishaji mwaka hu hakuma mtoto aliebaki kutokana  na ukosefu wa madarasa  amesisitiza Waziri Ndalichako.


Pia amezitaka Halmashauri zote nchini kuongeza kasi ya kutatua changamoto katika sekta ya elimu kwa kuweka mikakati ya ndani kwani fedha za miradi zinazopelekwa na Serikali ni kwa ajili ya kuongeza nguvu.


Aidha, Waziri amesema ili kurahisisha utendaji kazi wa Maafisa Elimu na Wathibiti ubora wa shule kufanya kazi kwa ufanisi, Serikali mwaka huu 2021 imenunua magari 165 yatakayosambazwa katika  Halmashauri nchini na mengine 66 kwa ajili ya wathibiti ubora wa shule yatakayosaidia kufanya ufuatiliaji wa taaluma katika maeneo yao.


Pia Profesa Ndalichako amezungumzia Mradi wa kuboresha elimu ya sekondari ambao utajenga shule za Sekondari 26 kwa ajili ya watoto wa kike  ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 hadi 1500 kila moja.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange amewataka wadau wa elimu katika Wilaya hiyo wakiwemo wazazi na viongozi mbalimbali katika ngazi zote kushirikiana kuanzisha hatua za ujenzi wa maboma ya miundombinu ya elimu katika Halmashauri za Wilaya Kasulu ili kuondoa changamoto ya  upungufu wa miundombinu mbalimbali ya kielimu


Amesisitiza kuwa katika mwaka huu 2021 kuanzia Julai; kwa kuanzia wanatarajia kufyatua matofali 200,000 kwa ajili ya maboma ya madarasa.


Mmoja wa wanafunzi aliyepata daraja la kwanza kutoka  shule ya sekondari Bogwe iliyopo wilayani Kasulu, Anitha Sunzu ameishukuru Serikali kwa kumpatia tuzo na kwa kuendelea kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania bila ya upendeleo huku akiwataka wanafunzi wengine kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu kwa walimu.

Post a Comment

Previous Post Next Post