*******************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAKAZI wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuwazuia watoto na wanafunzi wasiokote na kula nzige walivamia eneo hilo ambao walikufa kwa kupigwa dawa.
Pia, wafugaji wa maeneo yaliyovamiwa na nzige hao wametakiwa wasichunge mifugo yao kwenye maeneo yaliyopigwa dawa hadi angalau zipite siku tatu.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi ameyasema hayo wakati akielezea mikakati ya kupambana na nzige wavamizi.
Myenzi amesema nzige hao wamevamia wilaya hiyo kwenye kata ya Naberera katika vijijini vya Landanai na Losokonoi na dawa za sumu zinanyunyizwa kila walipotua ili kuwamaliza.
Amewataka wananchi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari ili wasipate madhara pindi dawa zenye sumu zitakapopulizwa katika maeneo yaliyovamiwa na nzige hao.
“Tuendelee kupeana ushirikiano na taarifa kila tukiwaona wadudu hao waharibifu na tuendelee kuelimishana watu wasiokote au kuka nzige hao kwani wana sumu kali,” amesema Myenzi.
Hata hivyo, amesema sehemu ya kundi la nzige hao imeruka kuelekea kijiji cha Naberera wakifuata usawa wa nguzo za nishati ya umeme ila wamefuatiliwa na wataalamu kwani waliingia ndani kidogo ya pori.
“Tumefanikiwa kupata ndege ambayo ilinyunyiza dawa ya sumu kwenye eneo la Losokonoi chini ya ujazo wa hekta 37 takribani ekari 100 na baadhi ya nzige wamekufa na wangine wanaendelea kufa kwa saa 72 zijazo,” amesema Myenzi.
Mkazi wa kijiji cha kijiji cha Landanai, Elipokea Estomy amemshukuru Myenzi na wataalamu wake kwa namna alivyotimiza wajibu wake katika kupambana na nzige hao wavamizi.
Amesema kutokana na jitihada hizo nzige hao wavamizi watamalizika haraka ili kunusuru mashamba ya wakulima mbalimbali wa eneo hilo.
Nzige hao wanadaiwa kutoka kwenye nchi za jangwa za Ethiopia, Eritrea na kaskazini ya Kenya na kufika Wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, baadhi ya maeneo ya wilaya ya Simanjiro na wilayani Longido mkoani Arusha.