…………………………………………………………………..
Viongozi wa Vyama vya
Ushirika nchini wametakiwa kutumia njia mbadala kulipa madeni ya
wanaushirika badala ya kuuza mali ili kulipa madeni hayo.
Kauli hiyo imetolewa
na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alieanza ziara ya kikazi
ya siku tatu leo ( 18.02.2021) mkoani Kilimanjaro ambapo amebaini
changamoto ya uwepo wa madeni katika vyama vingi vya ushirika hapa
nchini yaliyosababishwa na matatizo ikiwemo kukosekana kwa weledi
miongoni mwa viongozi wa ushirika.
Akiongea na bodi
pamoja na menejimenti ya kiwanda cha kahawa cha Moshi (TCCco )Kusaya
amesema vyama vingi vya ushirika vinadaiwa na watumishi wake kwa
kutolipa mishahara kwa muda mrefu hivyo ushirika utafute njia mbadala ya
kulipa madeni hayo badala ya kufikiria kuuza majengo ya ushirika na
Mali zingine.
“Tutafute namna bora
ya kulipa madeni ya wanaotudai kwa kuwa suluhu sio kuuza majengo
siamini kwamba kila anayedai tunauza jengo wakati kila mwaka atastaafu
mtumishi tutauza majengo mangapi alihoji” Katibu Mkuu Kusaya.
Hata hivyo ,Kusaya ametoa wito kwa kila Chama cha ushirika kilinde mali zake kwa ajili ya watu wake
Katika kuhakikisha
vyama vya ushirika nchini vinatekeleza wajibu wake Kusaya amewataka
wataalamu wa fedha kuhakikisha kwamba kila deni litakalolipwa kwa
mtumishi wa ushirika linakaguliwa na kubainika kwamba ni deni sahihi.
“Wataalam wa fedha ni
sharti wajiridhishe na uhalali wa madeni kwenye ushirika kabla malipo
hayajafanyika ili kuepuka madeni hewa ambayo Rais Dkt. John Pombe
Magufuli anapambana kuyadhibiti kwa maslahi ya wanaushirika wakiwemo
wakulima” alisisitiza Kusaya.
Katibu Mkuu huyo wa
Kilimo yupo kwenye ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi wa vyama vya
ushirika na kuhimiza Kilimo cha umwagiliaji na kuzungumza na watumishi
wakiwemo wakulima wa mazao mbalimbali ili kutatua changamoto
zinazowakabili.