TBS KAGERA YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUSAJIRI BIDHAA YA SENENE.

 

………………………………………………………………………………………………….
Na Silvia Mchuruza,Kagera.
SHIRIKA la viwango Tanzania (TBS) limewashauri wafanyabiashara wa senene mkoani Kagera kusajili bidhaa hiyo katika shirika hilo ili kuongezea thamani pamoja na kupanua masoko ya nje ya nchi.
Meneja uthibiti ubora daraja la pili (TBS) Mtukula mkoani Kagera, Vicent Mabula alieleza hayo katika mafunzo ya wajasiriamali wadogo na wakubwa mkoani humo iliyolenga kuwafundisha namna ya buongeza thamani biashara zao pamoja na kupanua masoko iliyofanyika katika ukumbi wa ELCT Bukoba Hoteli.
Mabula alisema alama ya TBS humdhibitishia mtumiaji kuwa bidhaa hiyo inafaa kwa matumizi hivyo uongeza thamani pia inaweka bidhaa husika katika usawa wa biashara ambao usaidia kuondoa mkanganyiko wa mmiliki.
“Katika ukanda wa biashara kuna makubaliano ya kidunia kupitia shirika la biashara la dunia ambapo TBS inaiwakilisha Tanzania katika shirika hilo, hivyo kama bidhaa yako imesajiliwa na TBS utakuwa na uwanja mpana wa kutanua masoko nje ya nchi.
Kama biashara itasajiliwa TBS itamsaidia mfanyabiashara kutanua masoko ndani na nje ya nchi kutokana na biashara hiyo kuaminiwa na watumiaji kwa maana kuwa bidhaa hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu,” alisema.
Wakati huo huo mwandaaji wa mafunzo hayo ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya Customer development limited, Emanuel Mwombeki alisema semina hiyo iliyoambatana na maonyesho ya biashara ya senene imelenga kuwafungulia fursa mbalimbali za biashara wa Mkoa wa Kagera.
“Licha ya semina hii kuitwa ‘Senene Festival’ lakini linawakutanisha wafanyabiashara wa senene na wajasiriamali wengine ili kubadirishana uzoefu, changamoto na kujadiliana ni jinsi gani wanaweza kuzitatua kwa ajili ya kuboresha biashara zao,” alisema.  
Naye Josephina Gosbeth ambaye ni mfanyabiashara wa senene alisema biashara hiyo inakabiliwa na changamoto ya soko pamoja na upatikanaji wa bidhaa hiyo msimu huu kuwa ngumu.
“Tunaomba serikali ituruhusu tujenge mabanda ya kudumu katika soko la senene ili tuweze kujikinga na mvua ambayo wakati mwingine inaponyesha inaambatana na upepo mkali na kusababisha tulowe sisi pamoja na bidhaa zetu.
Lakini pia upatikanaji wa senene msimu huu umekuwa mgumu kutokana na senene hao kutodondoka kwa wingi jambo linalotulazimu kuwalangua kwa bei kubwa kutoka kwa wafanyabiashara wachache ambao wana hazina ya kutosha na kutufanya tuwauze kwa bei kubwa jambo linalosababisha wateja kulalamika,” alisema Josephina.
Josephina ambaye maisha yake na familia yanategemea biashara ya senene alisema semina hiyo imemsaidia kujua jinsi ya kuisajili biashara ya senene ili kuiongezea thamani kwa ajili ya kupanua masoko ya nje na kuitumia biashara hiyo kuomba mikopo ili kuipanua zaidi.
Mwenyekiti wa wajasiriamali wa senene Manispaa ya Bukoba, Anastela Rwegarulila kutokana na bidhaa ya senene kuadimika mwaka huu, wafanyabiashara wa zao hilo wamejikuta wakilangua ndoo ya senene kwa shilingi 300,000 badala ya 100,000 jambo ambalo limesababisha biashara hiyo kuwa ngumu.
“Mwaka huu biashara ya senene imekuwa ngumu sana jambo ambalo limesababisha mitaji ya wafanyabiashara wengi kuyumba kutokana na kutumia mitaji mikubwa na kupata faida kidogo,” alisema.
Afisa Maendeleo ya Jamii ya Manispaa ya Bukoba, Murshid Issa amewashauri wafanyabiashara wa senene kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali ili kuboresha biashara zao.
“Niwasihihi wajiwekee malengo ya kuboresha biashara yao na waje tuwapatie mikopo inayotolewa na halmashauri ambayo haina riba ili iwasaidie kufikia malengo,” alisema.  

Post a Comment

Previous Post Next Post