KATIBU MKUU KUSAYA ATAKA MASHIKAMANO YA WIZARA ZA SEKTA YA KILIMO TANZANIA BARA NA VISIWANI KUWA NA TIJA ZAIDI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Tanzania Bara) Bwana Gerald Kusaya (Katikati) akiongea na Wataalam kutoka Wizara ya Sekta ya Kilimo akiwa pamoja na Mwenyeviti wa mkutano huo wa Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) Bi. Irene Lucas (kushoto) na Mwenyekiti mwenza kutoka Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasirli na Mifugo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Bwana Sheha Hamdan (Kulia) leo tarehe 10 Februari, 2020 katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo Jijini, Dar es Salaam

Mwenyekiti wa mkutano huo wa Wataalam; Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo (Bara) Bi. Irene Lucas akiwa sambamba na Mwenyekiti Mwenza Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti Bwana Sheha Hamdan wakiwaongoza mkutano huo leo.

Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Bwana Justine Japhet akiongea na Wataalam kutoka Wizara za Sekta ya Kilimo (Tanzaia Bara/ Visiwani) leo tarehe 10 Februali katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo, Jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo (Bara) wakifuatilia mkutano huo

Sehemu ya Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasirli na Mifugo (Visiwani) wakifuatilia mkutano huo.

………………………………………………………………………

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Tanzania Bara) Bwana Gerald Kusaya leo 10 Februari, 2021 ametembela mkutano wa Wataalam wa masuala ya Sera, Utafiti na Kilimo Mazao kutoka Wizara ya Kilimo (Tanzania Bara) na Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo (Tanzania Visiwani) na kuelekeza kuwa wanapaswa kuja na mikakati itakayolenga kuongeza tija na matokeo bora zaidi kwa ustawi wa Watanzania kutoka pande zote za Muungano.

Katibu Mkuu Kusaya ameyasema hayo baada ya kuwatembelea Wataalam hao ambao wamekutana kwa ajili ya mkutano wa kujadili mashirikiano kati ya Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasirli na Mifugo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) mkutano wa siku mbili unaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Kilimo Jijini Dar es Salaam kwa siku mbili.

Katibu Mkuu Kusaya ametoa wito kwa Wataalam hao kutoa majibu kwenye baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikikabili Sekta ya Kilimo (Mazao) na kuongeza kuwa Watanzania kutoka pande zote za Muungano wanataraji kunufaika na matokeo chanya kutoka kwenye Sekta za kiuchumi kama Kilimo na Uvuvi.

“Ndugu Washiriki; Kikao cha leo na kesho; Vitoe majibu ya changamoto kadhaa kwenye Sekta ya Kilimo; Mtanzania yoyote kutoka Bara na Visiwani aone utofauti na manufaa ya Sekta ya Kilimo katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano.” Amesema Katibu Mkuu Kusaya.

Awali Mwenyekiti wa mkutano huo wa Wataalam; Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo (Bara) Bi. Irene Lucas sambamba na Mwenyekiti Mwenza Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Sera na Utafiti Bwana Sheha Hamdan amesema mkutano huo utajikita katika maazimio kadhaa likiwemo azimio la kuendeleza ushirikiano kwenye eneo la utafiti, mafunzo na utoaji wa hakimiliki kwa ugunduzi wa mbegu.

Maazimio mengine ni pamoja na kutoa mafunzo ya pamoja kwa Wataalam na Wakulima kuhusu udhibiti wa visumbufu vya mimea/mazao hususan milipuko ya visumbufu.

Azimio lingine ni pamoja na kuendeleza ushirikiano kwenye eneo la umwagiliaji, zana za kilimo, sera na mipango pamoja na maenedeleo ya mazao.

Eneo lingine la maazimio ni pamoja na kuboresha mfumo wa uratibu wa mazao na taadhari ya awali (Crop Monitoring and Early WarrningSystem) kwa pande mbili. Kukamilisha mchakato wa utiaji saini ya makubaliano kati ya ZARI na TOSCI kwenye masuala ya udhibiti wa ubora wa mbegu.

Wakati huohuo Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Bwana Japhet Justine aliwaeleza Wataalam wa Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo kutoka (Tanzania Visiwani) ambao walitaka kufaham utaratibu wa kupata mikopo ya kuendeleza shughuli za maendeleo ya Sekta ya Kilimo hususan kilimo cha umwagiliaji, mifugo maliasili kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ipo kwa ajili ya Watanzania waliopo Bara na Visiwani.

Bwana Japhet amesema Benki ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ni Taasisi ya Umma na ipo Kimkakati kwa ajili ya kusaidi na kuendeleza sekta hizo za kiuchumi na kuongeza kuwa Benki hiyo imekuwa na ushirikiano wa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo mwaka 2019 Benki hiyo ilitoa mkopo wa shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya kugharamia ununuzaji wa karafuu kutoka kwa Wakulima kabla ya kuuzwa nje ya nchi.

Bwana Japhet Justine ameongeza kuwa Benki hiyo ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha miradi yote ya kilimo, mifugo na uvuvi ambayo ina sura ya kuwezesha Wananchi wengi kiuchumi kwa pamoja na kuongeza kuwa; Wananchi wanakaribishwa kuitumia Benki hiyo kwa ajili ya kupata mikopo yenye riba nafuu ya asilimia 9 kwa miradi mingi ukilinganisha na Benki nyingine za kibiashara.

“Hadi sasa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imekopesha zaidi ya shilingi bilioni 300 kwenye zaidi ya miradi 213 Tanzania Bara/Tanzania Visiwani na tunajivunia kuwa sehemu ya mafaniko ya ujenzi wa uchumi wa Watanzania wengi.” Amekaririwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TABD) Bwana Japhet Justine.

Post a Comment

Previous Post Next Post