HALI YA MAJI KWA BWAWA LA MTERA INARIDHISHA – DKT. KYARUZI

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi leo Februari 14, 2021 amesema hali ya maji katika bwawa la kuzalisha umeme la Mtera inaridhisha.

Dkt. Kyaruzi amesema hayo katika ziara ya kukagua mitambo ya kufua umeme ya Mtera ambayo ipo kati ya Iringa na Dodoma.

Aidha, Dkt. Kyaruzi amesema hali ya ufuaji umeme katika kituo cha Mtera inaridhisha na mashine zote mbili zinafanya kazi.

“Imekuwa faraja kwetu Mtera inazalisha kama tulivyotegemea, vile vile tumefarijika sana kuona bwawa letu ambalo linahifadhi maji kwa ajili ya kufua umeme lina maji ya kutosha yatakapo tupeleke mwaka huu 2021 na 2022” amesema Dkt. Kyaruzi.

Awali akiikaribisha Bodi kwa niaba ya Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Meneja Uzalishaji Umeme, Mhandisi Manfred Mbyallu amesema mitambo ipo katika hali nzuri na yote inafanya kazi.

“mitambo ya Mtera ipo miwili ambapo kila mmoja unauwezo wa megawati 40 hivyo kufanya jumla ya megawati 80″ameongeza Mhandisi Manifred.

Meneja wa kituo cha kufua umeme cha Mtera, Mhandisi Elias Mwalupilo akitoa wasilisho kwa Bodi amesema kina cha maji bwawa la Mtera kimeongezeka kama ilivyo rekodiwa leo Februari 14, 2021 na kufikia mita za ujazo 697.97 juu ya usawa wa bahari.

Amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha bwawa limebakiza mita 0.53 kufika kina cha juu ambacho ni mita 698.50.

Bwawa la Mtera ndilo inalotumika kufua umeme kwenye vituo vya Mtera na Kidatu ambapo linapata maji kupitia vyanzo vya mto Ruaha Mkuu, Ruaha Mdogo na Kisigo.

Akihitimisha ziara hiyo Dkt. Kyaruzi ametoa wito kwa wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa vyanzo vya maji kuhakikisha shughuli hizo hazileti athari katika upatikanaji wa maji na wayatumie kulingana na maelekezo yanayotolewa na wataalamu kutoka Bonde la Mto Rufiji.

Ameongeza mradi wa Julius Nyerere ukikamilika utategeme maji yanayotoka Mtera pia, hivyo kuathirika kwa Mtera kutaathiri ufuaji wa umeme Julius Nyerere.

Post a Comment

Previous Post Next Post