WAZIRI UMMY MWALIMU NA WAZIRI GEOFFREY MWAMBE WATEMBELEA KIWANDA CHA BTY

 

………………………………………………………………………….

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe wametembelea kiwanda cha BTY cha kurejeleza betri za magari kwa ajili ya kupata malighafi za kutengeneza betri na bidhaa zingine za plastiki. Mawaziri hao waliambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Profesa Esnath Chaggu, Mkurugenzi Mkuu wa (NEMC) Mhandisi Daktari Samuel Gwamaka, pamoja na Wataalamu kutoka NEMC.

Akiongea na Waandishi wa Habari katika kiwanda hicho kilichopo Buguruni jijini Dar es Salaam Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa mwekezaji hakuandaa mpango wa usimamizi wa ardhi kulingana na bidhaa anazozitengeneza kama vile utiririshaji wa maji taka, vumbi wakati wa uzalishaji hali inayopelekea uchafuzi wa Mazingira.

“Nimetoa maelekezo kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kukaa na Mwekezaji kuangalia ni namna gani wafanye ili kuepuka madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira, uwekezaji uende sambamba na kuhakikisha Sheria ya Mazingira zinafuatwa ili kulinda Afya zetu na Mazingira kwa ujumla.”

Mhe. Ummy mwalimu ameongeza kuwa Kiwanda cha BTY kinahitajika, lakini ni lazima kizingatie mifumo ya Usimamizi wa Mazingira kwasababu madini yanayotokana na urejelezwaji wa hizo betri yana athari kwa mazingira na yanaweza kusababisha saratani na magonjwa mengine kama hakuna udhibiti endelevu katika usimamizi wa mazingira.

“Kiwanda tunakihitaji lakini lazima kizingatie taratibu na sheria za mazingira ili kuepusha madhara yanayotokana na kemikali zinazotokana na hizi betri wakati wa urejelezwaji, kiwanda kinalipa kodi ya Serikali na kimeajiri Watanzania wengi lakini hiyo haitoshi kama hakizingatii Sheria za mazingira zinasemaje katika uwekezaji.”

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Geoffrey Mwambe amesema kuwa uwepo wa kiwanda cha BTY ni muhimu kwasababu unasaidia kusafisha mazingira kwenye suala zima la ukusanyaji wa betri mbovu kwa ajili ya kurejeleza tatizo ni namna ambavyo kinachakata hizi betri ni katika hali ambayo si rafiki kwenye mazingira, hawajafuata taratibu za usimamizi wa mazingira kama inavyotakiwa.

“Kiwanda cha BTY kina faida hasa katika kupunguza takataka za betri kwenye mazingira yetu kwasababu wanazikusanya na kuzirejeleza, lakini wanapaswa kuelekezwa namna bora ya utendaji kazi wao ili wasiharibu mazingira. Nchi yetu inahitaji Viwanda vingi ili viendelee kutoa ajira kwa vijana wetu na pato letu la Taifa liongezeke kwasababu wanalipa kodi, lakini pamoja na hayo suala la utunzaji wa Mazingira ni lazima lifuatwe kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.”

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Daktari Samuel Gwamaka amesema wamiliki wa viwanda Tanzania wajitahidi kupata Wataalamu elekezi wa Mazingira wenye uwezo wa kuwasaidia kuwashauri vizuri kuhusu mazingira wakati wa uwekezaji. Na pia amewataka wawekezaji waende Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira pale wanapopata changamoto za kupata Wataalamu elekezi wa Mazingira ili kuepuka kufungiwa au kupigwa faini.

“Natoa rai kwa wenye viwanda kuzingatia kupata Wataalamu elekezi wa mazingira wenye uwezo wa kuwashauri namna nzuri ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira wakati wa uwekezaji, pia napenda kuwakaribisha Ofisi za NEMC pale wanapopata changamoto katika kuchagua wataalamu elekezi ili tuweze kuwashauri ili kuepuka usumbufu katika kazi zao.”

Post a Comment

Previous Post Next Post