TSC YAWAAGA WASTAAFU WAKE

 

Katibu Mstaafu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindura (kulia), akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba, wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu wa Tume, iliyofanyika Januari 26, 2021, mjini Morogoro. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Willy Komba, akitoa hotuba ya kufunga Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume, mjini Morogoro, Januari 26, 2021. Kushoto ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Katibu Mstaafu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindura, akizungumza na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo, wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu iliyofanyika Januari 26, 2021 mjini Morogoro.

Baadhi ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC),  waliostaafu na wanaotarajiwa kustaafu hivi karibuni, wakiungana na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume, kuimba kwa furaha wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wastaafu hao iliyofanyika Januari 26, 2021 mjini Morogoro.

Watumishi mbalimbali wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) waliostaafu na wanaotarajiwa kustaafu hivi karibuni, wakipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume, Profesa Willy Komba, wakati wa hafla fupi ya kuwaaga iliyofanyika mjini Morogoro, Januari 26, 2021.

****************************************************

Na Veronica Simba – TSC

Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imewaaga rasmi watumishi wake 10 waliostaafu na wale wanaotarajiwa kustaafu hivi karibuni, akiwemo aliyekuwa Katibu wa Tume, Winifrida Rutaindura.

Tukio hilo lilifanyika Januari 26, 2021 mjini Morogoro, wakati wa kuhitimisha Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliohudhuriwa na Mwenyekiti wa Tume, Profesa Willy Komba, Kaimu Katibu wa Tume, Moses Chitama, Menejimenti na wawakilishi kutoka wilaya zote za Tanzania Bara.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo fupi, Profesa Komba aliwapongeza wastaafu hao kwa utumishi uliotukuka na kuwaomba waendelee kuwa Mabalozi wa Tume kokote watakakokwenda.

Kwa upande wake, Katibu Mstaafu wa Tume, Bibi Rutaindura, akizungumza kwa niaba ya wastaafu wenzake, alishukuru ushirikiano walioupata kutoka kwa watumishi wote na kuwaasa kuendeleza mshikamano baina yao.

Akitoa hotuba ya kufunga Mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi, Profesa Komba alibainisha kuwa umekuwa wenye mafanikio makubwa huku akiwakumbusha wajumbe kuzingatia maadili ya kazi na weledi ili kuiwezesha Tume kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali.

“Nawasisitiza muendelee kufanya kazi kwa weledi ili tufikie malengo na kuwa Taasisi ya mfano wa kuigwa kwa kuihudumia vyema kada ya walimu na hivyo kuwezesha kuinua zaidi kiwango cha elimu nchini.”

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwakumbusha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuondoa uzembe na vitendo vya rushwa mahali pa kazi pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima, hivyo akawataka kujiepusha na vitendo hivyo badala yake kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo.

Wastaafu wengine walioagwa ni pamoja na Christina Hape aliyekuwa Makao Makuu Dodoma, Corona Maira (Ilemela), Anna Mutungi (Bukoba), Fanuel Edward (Musoma), Rahim Mgongo (Lushoto) na Vicent Shemsanga (Kibaha).

Wengine ni Matilda Philemon (Kigoma), Elineema Mtaita (Morogoro) na Magdalena Nakitundu (Tabora).

Mkutano huo wa siku mbili wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu, ulifunguliwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde.

Post a Comment

Previous Post Next Post