SERIKALI YATOA MIEZI 3 KWA WENYE VIFUNGASHIO VISIVYOKIDHI VIWANGO VYA TBS VIONDOLEWE SOKONI

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu akionesha vifungashio vya plastiki vilivyogeuzwa matumizi na kutumika kama vibebeo vilivyopigwa marufuku wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Januari 8, 2021

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 8, 2021 jijini Dodoma kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu leo Januari 8, 2021 jijini Dodoma kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Joseph Sokoine.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 8, 2021 jijini Dodoma kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa.

…………………………………………………………………………..

Serikali imetoa miezi mitatu kwa wenye shehena ya vifungashio visivyokidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) vinaondolewa sokoni.

Agizo hilo limetolewa leo Januari 8, 2020 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Ofisi hiyo jijini Dodoma kuhusu matumizi ya vifungashio vya plastiki kutumika kama vibebeo vya bidhaa.

Ummy alisema hatua hiyo ya Serikali imechukuliwa baada ya kuwepo kwa vifungashio vinavyotumika kama vibebeo vilivyozagaa madukani, sokoni na maeneo mbalimbali.

Alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana kutokana na katazo la mifuko ya plastiki siku za hivi karibuni kumejitokeza changamoto ya matumizi ya vifungashio vya plastiki aina ya tubings visivyokuwa na sifa na hivyo kutokukidhi matakwa yaliyowekwa na TBS.

Aidha, Waziri Ummy aliongeza kuwa vifungashio hivi kwa sasa vinazalishwa kwa wingi na kwa ukubwa mbalimbali na vimekuwa vikitumika kama mifuko ya kubebea bidhaa sokoni na kuleta dhana kuwa mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku imerudi kivingine kama “vifungashio”.

Alisema mifuko hii imeanza kuzagaa kwenye mazingira ya mitaa yetu na vijiji vyetu kwa kasi kubwa,  na hivyo kurudisha nyuma mafanikio makubwa tuliyoyapata katika kipindi chote cha kupambana na changamoto ya mifuko ya plastiki. 

Kwa mantiki hiyo Waziri Ummy aliwataka wasambazaji, wazalishaji wa vifungashio hivi na waagizaji kuacha mara moja kuzalisha, kusambaza, kuuza na kutumia vifungashio hivyo na kusisitiza kuwa baada ya kipindi hicho Serikali haitatoa tangazo lingine lolote kuhusiana na katazo la matumizi ya vifungashio visivyokuwa na ubora.

 

Waziri huyo alisema Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu kisheria na katika kipindi hiki tunaendelea na operesheni maalumu kuwabaini wanaokwamisha mafanikio haya kwa kuzalisha na kusambaza vifungashio hivyo na hatutawavumilia watu hawa.

“Sitaki kuwaathiri wafanyabiashara wadogo wadogo ambao kwangu mimi ndio wananchi ninaotaka kutowaathiri, maana tukisema piga marufuku hizi karoti anaweka wapi hizi nyanya anaweka wapi ubuyu, kwa hiyo lengo la Serikali kuweka miezi mitatu ni kuzingatia hali halisi ya wafanyabiashara ndogondogo ambao ndiyo maana ni watumiaji wa mwisho hivyo tunataka kuwabana twazalishaji ili wanaonunua wanunue vifungashio vyenye ubora,” alisisitiza.

“Napenda kuwakikishia wananchi kuwa Serikali kupitia TBS inayo kanzidata ya wazalishaji wa kutosha wa vifungashio vinavyokidhi viwango na hivyo hapatakuwa na uhaba wa vifungashio vinavyokidhi viwango baada ya kipindi hicho cha miezi mitatu. 

Nitumie nafasi hii kuwaasa wazalishaji na wawekezaji wa ndani kuchangamkia fursa hii kwa kuzalisha vifungashio vyenye kukidhi viwango nilivyobainisha,” alisema.

Akizungumzia kuhusu katazo la mifuko ya plastiki Waziri Ummy alisema utekelezaji wa katazo hilo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kipindi chote cha mwaka mmoja na nusu tangu Serikali ilipotoa tangazo hilo. 

Alitaja mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano wa wananchi, taasisi, waliokuwa wazalishaji na wasambazaji na makundi mbalimbali yaliyoshiriki katika kuzingatia maelekezo ya Serikali katika kupambana na changamoto ya mifuko ya plastiki.  

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo alisema Ofisi hiyo itashirikiana na TBS kuanza kampeni ya kupitia tena mifuko ya ‘non woven’ kwani kuna uwezekano wa kuwepo kwa mifuko isiyo na viwango. 

Malongo alisema Serikali ilipoweka katazo la mifuko ya plastiki iliweka pia viwango vya mifuko ya aina hiyo akitaja kuwa ni lazima iwe na uzito wa gramu 70 kwa mita ya mraba moja ili itumike kwa zaidi ya mara moja.

Aliongeza kuwa pia lazima mifuko hiyo iwe na nembo ya TBS ili kuonesha kuwa imekidhi vigezo vinavyotakiwa pamoja na kutambulisha jina la mzalishaji.

Kigezo Kingine ni viwe na lakiri (Seal), ikimaanishwa kuwa kifungashio kinatakiwa kifungashwe na anayefungasha bidhaa yake ili kuuza kabla ya kwenda sokoni.

Post a Comment

Previous Post Next Post