NAIBU WAZIRI WA MAJI AENDESHA ZOEZI LA UPANDAJI MITI MBEYA

 

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akipanda mti kuashiria uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika Jiji la Mbeya

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akipanda mti kuashiria uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika Jiji la Mbeya

………………………………………………………………………………….

Na Evaristy Masuha

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (MB) ameziagiza Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira pamoja na wadau wa maji kote nchini kuhakikisha wanapanda miti ili kutunza vyanzo vya maji. Agizo hilo amelitoa Januari 11wakati akizindua zoezi la upandaji miti lililoendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  jijini Mbeya (Mbeya UWSA). Amesema maji ni uhai na njia nzuri ya kuhakikisha vyanzo vya maji vinaendelezwa ni kupanda miti rafiki kwa mazingira. 

Aidha amewapongreza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Mbeya kwa kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji kikiwemo chanzo cha maji cha Nzovwe ambacho kinatoa zaidi ya asilimin 40 ya maji yanayosambazwa sehemu mbalimbali jijini mbeya.

 Awali akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji kwa mji wa Mbeya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya Mhandisi Ndele Mengo amesema mahitaji ya maji kwa jiji la Mbeya ni lita za ujazo milioni 70 kwa siku ambapo Mamlaka kwa sasa inazalisha lita za ujazo milioni 40 kwa siku. 

Amesema Mamlaka inaendelea na ujenzi wa miradi mipya ambayo itasaidia kwa kliasi kikubwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji. Miradi hiyo ni pamoja na  mradi wa Maji wa  Mwashaali, Shongo, itende, Nzovwe-isyesye, Itezi pamoja na kuboresha vyanzo vingine vya maji.

Kwa upande wake Chifu Mkuu wa Jiji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Chifu Roketi Masoko Mwashinga ameishauri Serikali kuwafikisha wote wanaokiuka maagizo ya utunzaji vyanzo vya maji kwenye mahakama ya jadi. 

“Waleteni kwetu. Sisi ni Mapilato. Tutawashughulikia”. Amesema chief Mwashinga.

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya inatarajia kupanga miti milioni sita kwa mwaka 2021 ikiwa ni mwendelezo wa zoezi la upandaji miti linalofanyika kila mwaka.

Post a Comment

Previous Post Next Post