NAIBU WAZIRI BYABATO AIAGIZA TANESCO KUKAMILISHA UTENGENEZAJI WA MTAMBO NDANI YA WIKI MBILI

 

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akizungumza na Mbunifu wa Mtambo wa kufua umeme kwa kutumia sumaku Bw. Rojers Msuya (52) Mkazi wa Kawe, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar-es-salaam. Mtambo unaoonekana hapo chini katika picha una uwezo wa kuzalisha umeme KVA 5 sawa na WATT 5000. 

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akisoma kipimo cha umeme kinachotumika kupima kiwango cha umeme kinachozalishwa kwenye mtambo wa kufua umeme kinachoitwa (Clamp digital meter) kipimo hicho kimethibitisha kuwa, umeme unaozalishwa na mtambo uliobuniwa na Mbunifu Rojers Msuya unakidhi viwango vyote vya TANESCO.

Naibu Waziri Byabato, akiwa pamoja na Kamishna Msaidizi wa Umeme – Wizara ya Nishati, (aliyemwakilisha Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati.) Naibu Mtendaji Mkuu wa TANESCO(aliyemwakilisha Mtendaji Mkuu TANESCO) wakiwa na wataalam wengine kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO pamoja na timu ya waandishi wa Habari, leo tarehe 25 Januari, 2021 wamemtembelea Mbunifu wa Mtambo huo wa kufua umeme kwa njia ya Sumaku na kujionea namna mtambo huo unavyofanya kazi

Rojers Msuya (52) Mkazi wa Kawe, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar-es-salaam ambaye ni Mbunifu wa Mtambo wa kufua umeme kwa kutumia sumaku akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 25 Januari, 2021 nyumbani kwake Kawe jijini Dar-es- salaam mara baada ya Kutembelewa na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato. 

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato akipata maelezo kutoka kwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji – Usafirishaji wa TANESCO Mha. Isaac Chanji (akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO). Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Umeme wa Wizara ya Nishati, Mha. Innocent Luoga, mara baada ya kuwasili Kawe jijini Dar-es-salaam kwa lengo la kukutana na Mbunifu wa ufuaji umeme kwa kutumia sumaku. 

………………………………………………………………………………………….

Na Dorina Makaya – Dar-es-salaam.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, ameiagiza TANESCO kushirikiana na Mbunifu wa Mtambo wa Kufua umeme kwa kutumia sumaku kutengeneza Mtambo mwingine mpya ndani ya wiki mbili.

Naibu Waziri Byabato ametoa maelekezo hayo leo tarehe 25 Januari, 2021 alipomtembelea Mbunifu huyo Bw. Rojers Msuya (52) nyumbani kwake Kawe, jijini Dar-es-salaam kushuhudia ubunifu wake wa kutengeneza mtambo wa kufua umeme kwa kutumia sumaku baada ya kupata taarifa kuhusiana na mbunifu huyo.

Naibu Waziri Byabato amesema, gharama zote za kutengeneza Mtambo huo, zitagharamiwa na Serikali kupitia shirika lake la TANESCO.

Naibu Waziri Byabato ameelezea kufurahishwa kwake na ubunifu huo na kusema kuwa kufanikiwa kutengeneza mtambo wenye uwezo mkubwa wa kufua umeme kwa kutumia sumaku kutawezesha maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme wa TANESCO na REA kupata umeme kwa gharama nafuu.

Naibu Waziri Byabato amemhakikishia Bw. Rojers Msuya kuwa, teknolojia ya kutengeneza mtambo wa kufua umeme kwa kutumia sumaku ikifanikiwa, atahakikisha Haki miliki zake zote kuhusiana na ugunduzi huo zinalindwa na kuhakikisha kunakuwepo na mikataba ya kisheria katika kushirikiana na TANESCO katika kutengeneza mitambo hiyo.

Naye Mbunifu huyo wa Mtambo wa kufua umeme kwa kutumia sumaku Bw. Rojers Msuya, amemweleza Naibu Waziri Byabato kuwa, Mtambo alioutengeneza una uwezo wa kuzalisha KVA 5 sawa na WATT 5000 na kuwa endapo atapata ushirikiano kutoka Serikalini itawezesha kupanua teknolojia hiyo aliyoibuni ya kufua umeme kwa kutumia sumaku.

Bw. Rojers amemweleza Naibu Waziri Byabato kuwa, hadi sasa, tayari amekwishatengeneza mashine 10 za majaribio za kufua umeme kwa njia ya sumaku na kuwapatia watu mbali mbali kuifanyia majaribio mitambo hiyo na hakuwahi kupata malalamiko yoyote kutoka kwa watumiaji hao kwa kipindi cha miaka minane sasa.

Bw. Rojers amesema sifa za Mitambo hiyo aliyoibuni ni kuwa haina kelele, haichafui mazingira na inaweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 bila ya kufanyiwa matengenezo.

Bw. Rojers amemshukuru Naibu Waziri Byabato pamoja na viongozi wengine wa Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kumtembelea na kujionea ubunifu wake.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Stephen Byabato, aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mha. Innocent Luoga (aliyemwakilisha Kamishna wa Umeme Wizara ya Nishati), Naibu Mkurugenzi Mtendaji – Usafirishaji wa TANESCO, Mha. Isaac Chanji (aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO), Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO pamoja na timu ya Waandishi wa Habari.

Post a Comment

Previous Post Next Post