*************************************************
Tanzania imekuwa kinara katika kufungua milango kwa wageni baada ya juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali na Sekta binafsi katika kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa korona, kujiandaa na kujitangaza kwa njia mbalimbali. Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania na kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii ndani na nje ya nchi inaendelea kutumia mbinu mbalimbali kujenga imani kwa wageni kuwa Tanzania iko salama na ndiyo kituo bora zaidi cha utalii katika bara la Afrika. Moja ya hatua zinazochukuliwa kwa sasa ni kutumia watu maarufu na mashuhuri duniani ambao wana ushawishi mkubwa na kupitia kwao dunia itaweza kufahamu zaidi kuhusu Tanzania.
Katika moja ya hatua za kufanikisha hayo, Bodi ya Utalii kwa kushirikiana na Balozi wa Hiari wa Utalii Bw. Nick Reynolds (Maarufu kama Bongozozo) na wadau wa sekta binafsi katika tasnia ya utalii wanaratibu ziara ya Bw. Drew Binsky muandaaji maarufu wa taarifa na makala za utalii duniani ambaye hutumia mfumo wa video kuwasilisha ujumbe wake. Bw. Drew Binsky ni raia wa Marekani ambaye huwasilisha taarifa kupitia mitandao yake ya kijamii yenye idadi kubwa ya wafuasi Facebook (milioni 3.4) Youtube (milioni 2.1) Snapchat (Laki 165) Instagram (Laki 530) na Twitter (Elfu 65). Kwa sasa video zake kwa ujumla zimeweza kufikia idadi ya watu bilioni moja wanaozitazama duniani.
Bw. Binsky anategemewa kuwasili nchini tarehe 27 Desemba, 2020 saa 4 asubuhi kupitia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, ambapo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) Waziri wa Maliasili na Utalii anategemea kuongoza mapokezi yake. Katika ziara yake hapa Tanzania anategemea kutembelea Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na kumalizia ziara yake katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ambao anapanga kupanda katika siku za baadaye